Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais Rouhani ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad bin Khalifa Aal Thani. Ametilia mkazo udharura wa kutatuliwa masuala na migogoro ya eneo hilo kupitia njia ya mazungumzo na kuongeza kuwa: Ni hatari sana kuwepo kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hili.
Rais Hassan Rouhani pia amelipongeza taifa na serikali ya Qatar kutokana na kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani na kutilia mkazo muhimu wa kuimarishwa zaidi na kustawishwa uhusiano wa Tehran na Doha katika nyanja zote hususan biashara na uchumi.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza misimamo ya serikali ya Qatar kuhusiana na masuala ya kanda ya Magharibi mwa Asia na kusema kuwa, njia pekee yenye mafanikio kwa ajili ya kudhamini usalama, amani na utulivu wa eneo hili ni ile ya kutumia njia za amani, kuwajibika na kutilia maanani maslahi ya pande zote. Amesisitiza kuwa, sera za kijeshi haziwezi kutatua matatizo ya Magharibi mwa Asia.
Wakati huo Rais Rouhani amesema kuwa, njia pekee itakayoiwezesha Marekani kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kufuta vikwazo vyake vyote na kutekeleza majukumu yake kwa msingi wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; wakati huo ndipo Iran itakapotekeleza majukumu yake ndani ya makubaliano hayo.
Kwa upande wake Amir wa Qatar pia ametoa pongezi kwa mnasaba wa kuwadia mwezi wa Ramadhani na kusisitiza udharura wa kustawishwa zaidi uhusiano wa nchi mbili. Sheikh Tamim bin Hamad bin Khalifa Aal Thani amesema Iran na Qatar zinapaswa kutumia uwezo wao wote kwa ajili ya kuimarisha zaidi mahusiano yao.
342/