3 Septemba 2021 - 11:13
Zaidi ya watu bilioni 4 duniani bado hawana Bima ya Jamii

Licha ya kuongezeka wigo wa bima au hifadhi ya jamii ulimwenguni wakati wa janga la corona au COVID-19, lakini zaidi ya watu bilioni 4 duniani kote bado hawana kabisa bima hiyo, imesema ripoti mpya ya Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa, ILO.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano inasisitiza kuwa hatua za kupambana na janga la COVID-19 hazikuwa za kutosha na zilikuwa za kutatanisha, zikipanua zaidi pengo kati ya nchi zenye kipato cha juu na kipato cha chini, na zimeshindwa kutoa ulinzi wa kijamii unaohitajika ambao kila mwanadamu anastahili.

Ripoti inasema ulinzi wa jamii ni pamoja na upatikanaji wa huduma za afya na usalama wa kipato, haswa kwa wazee, na pia ikiwa kuna ukosefu wa ajira, magonjwa, ulemavu, ajali kazini, uzazi au kifo cha mlezi mkuu wa familia, na pia kwa familia zilizo na watoto.

Mkurugenzi mkuu wa ILO, Guy Ryder amesema katika ripoti hiyo kwamba: “Nchi ziko njiapanda. Huu ni wakati muhimu wa kuchukua hatua za kupambana na janga hilo na kujenga kizazi kipya cha mifumo ya haki za ulinzi wa jamii.”

342/