Kwa mujibu wa IRNA, Masoud Satayshi, Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran, aliyasema hayo Jumanne katika mkutano na waandishi wa habari kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa tatu wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na kuongeza kwamba wahusika wa mauaji ya jenerali huyo na wenzake wanafuatiliwa kisheria na hadi sasa nyaraka 11 za kisheria zimetumwa katika nchi 9.
Satayshi amefafanua kuwa Shahidi Soleimani alikuwa nembo ya kupinga uistikbari katika uga wa kimataifa na sambamba na siasa za kupambana na dhulma za Jamhuri ya Kiislamu alizidisha kina cha nafasi ya kistratijia ya Iran katika nchi ambazo ni mhimili wa muqawama.
Akirejelea kufuatiliwa masuala ya kisheria na jinai katika kadhia ya Shahidi Soleimani, Msemaji wa Vyombo vya Mahakama vya Iran ameongeza kuwa hadi sasa mashtaka manne dhidi ya wahusika wa mauaji ya Shahidi Soleimani yametambuliwa kwa mujibu wa sheria za ndani na viwango vya kimataifa.
Jana Jumanne, tarehe 3 Januari 2023, ilikuwa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Siku hii nchini Iran huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Muqawama (Mapambano).
Lt. Jenerali Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Naibu Kamanda Jeshi la Kujitolea la Wannachi wa Iraq (PMU) Abu Mahdi al-Muhandis, na wanamapambano wenzao waliuawa shahidi katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mapema Januari 3, 2020. Shahidi Soleimani alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.
Ikulu ya White House na Pentagon ilitangaza kuwa ilihusika na mauaji hayo ya kigaidi na kuthibitisha kuwa shambulio hilo lilitekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa Marekani wa wakati huo Donald Trump.
Mipango mbalimbali imepangwa kuandaliwa nchini Iran, Iraq na nchi nyingine kadhaa ili kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kishahidi cha Jenerali Soleimani, al-Muhandis na wanajihadi wenzao.
342/