29 Agosti 2023 - 17:21
 Serikali ya Niger yazikatia umeme, maji na chakula balozi wa Ufaransa

Serikali ya mpito nchini Niger imezikata maji na umeme balozi za Ufaransa katika mji mkuu Niamey na ubalozi mdogo wa dola hilo la kikoloni ulioko Zinder na kupiga marufuku kupelekwa chakula kwenye balozi hizo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Msaada ya Baraza la Taifa la Kulinda Nchi (CNSP), Elh Issa Hassoumi Boureima, amewataka washirika wote wa vituo vya Ufaransa nchini Niger kusimamisha usambazaji wote wa maji, umeme na bidhaa za chakula.

Vilevile amesema, mtu au upande wowote utakaoendelea kuwasaidia Wafaransa katika kusambaza bidhaa na huduma zozote zile watahesabiwa kuwa ni "maadui wa watu huru wa Niger."

Taarifa hiyo imetolewa baada ya muda wa siku mbili uliotolewa na utawala wa kijeshi wa kumtaka balozi wa Ufaransa awe ameondoka nchini humo, kumalizika siku ya Jumapili. Wizara ya Mambo ya Nje ya Niger ilimpa Balozi wa Ufaransa nchini humo, Sylvain Itte, muda wa saa 48 za kuondoka katika ardhi ya Niger.Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Ufaransa kuendeleza fikra zake za kikoloni na kutoheshimu amri za serikali mpya ya Niger iliyoingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi yaliyompindua Rais Mohamed Bazoum ambaye wananchi wa Niger wanasema alikuwa kibaraka mkubwa wa Ufaransa.

Hayo yameripotiwa huku taarifa nyingine zikisema kuwa, maelfu ya wananchi wa Niger wamefanya maandamano karibu na kambi ya jeshi la Ufaransa katika mji mkuu Niamey kwa lengo la kutangaza uungaji mkono wao kwa serikali ya kijeshi na kutaka wanajeshi wa Ufaransa waondoke mara moja katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Waandamanaji hao walikusanyika karibu na kambi ya jeshi la Ufaransa katika mji mkuu siku ya Jumapili na kupeperusha bendera za Niger na kubeba mabango yenye kauli mbiu za kupinga Ufaransa kama inayosema: "Hatutaki jeshi la Ufaransa nchini Niger" na "Waache Wafaransa waondoke."

342/