Helikopta iliyombeba Seyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ujumbe aliofuatana nao, ambao Jumapili tarehe 19, Mei, 2024, walielekea Azerbaijan Mashariki kukagua Bwawa la Khoda Afarin na kuzindua miradi kadhaa ya kitaifa na ya kimkoa, ilipata ajali na kuanguka wakati ikitoka kwenye eneo la bwawa hilo kuelekea Kiwanda cha Usafishaji Mafuta cha Tabriz kutokana na hali mbaya ya hewa iliyokuwepo katika eneo la Varzghan.
Katika ajali hiyo chungu ya ndege, Rais Ebrahim Raisi na walioandamana naye, akiwemo Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, Ayatullah Seyyed Mohammad Ali Al-Hashem, Imamu wa Ijumaa wa Tabriz, Malik Rahmati, Gavana wa Azerbaijan Mashariki pamoja na timu ya walinzi wa rais, marubani na maafisa wa ndege wote walikufa shahidi katika tukio hilo la kusikitisha.Seyyed Ebrahim Raisi, rais wa nane wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita amekuwa akisimamia muhimili wa utendaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, daima alifanya juhudi kubwa za kustawisha nchi na kuendeleza uhusiano na nchi jirani, Waislamu na kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa na wasio na ulinzi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Katika mkondo huo huo siku ya Jumapili asubuhi na saa kadhaa kabla ya vifo vyao, wakati wa sherehe ya kufunguliwa bwawa hilo la pamoja katika mto wa mpakani wa "Aras", sherehe ambayo pia ilihudhuriwa na Rais Ilham Aliyev wa Jamhuri ya Azerbaijan, Rais Raisi alisema kuwa uhusiano wa kirafiki kati ya Iran na Azerbaijan ni imara na ambao umekita mizizi katika historia na imani za mataifa haya mawili na kamwe hauwezi kuvunjika.
Kuongezeka ushirikiano na nchi jirani na za kanda ilikuwa moja ya vipaumbele vya sera za nje za serikali ya 13 ya Rais Ebrahim Raisi, na alijaribu sana kukuza uhusiano na nchi hizo kupitia safari nyingi alizofanya katika nchi hizo, suala ambalo alilifanikisha kwa kiwango kikubwa.
Uwezo mkubwa wa kiuchumi wa nchi jirani na masuala ya pamoja ya kiutamaduni, kilugha na kidini ni miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele na Rais Ebrahim Raisi katika njia ya kupanua ushirikiano na nchi hizo.
Safari za Raisi katika miaka mitatu iliyopita katika nchi za Saudi Arabia, Pakistani, Uturuki, Iraq, Tajikistan, Turkmenistan, Russia, Qatar, Oman, Uzbekistan, Kazakhstan, China na Syria zote zinaonyesha imani aliyokuwa nayo katika kuendeleza uhusiano na nchi jirani, za kikanda na za Kiislamu.Mafanikio mengine ya safari hizo za Rais Raisi, ni kubainisha misimamo ya kuzingatia zaidi nchi za Mashariki katika sera za nje za serikali ya 13. Katika hotuba yake ya kwanza rasmi baada ya kushinda uchaguzi huo, Ebrahim Raisi alisisitiza kuwa, mtazamo wa sera za nje za serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kulinda maslahi ya kitaifa katika uga wa kieneo na kimataifa kwa kuimarisha uhusiano na nchi jirani, za eneo na za Kiislamu.
Katika safari zake mjini New York na katika mikutano ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa (UN) Raisi, aliunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni na kusisitiza mara kwa mara kuwa suluhu pekee ya tatizo la Palestina ni kukomeshwa ubaguzi na ukaliaji mabavu wa ardhi za Wapalestina na kuundwa nchi huru ya Palestina, mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu.
Akiashiria siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chake kipya Rais Ebrahim Raisi, alisisitiza kuwa ushirikiano wa kieneo una manufaa kwa amani, usalama na maendeleo ya mataifa ya eneo, jambo ambalo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalikaribisha.
Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye kama alivyokuwa Raisi, alisisitiza sana udharura wa nchi jirani kuishi pamoja kwa amani, amekuwa na nafasi kubwa katika kuimarisha uhusiano wa Iran na nchi jirani na za eneo, hususan na Saudi Arabia na kusema kuwa urafiki na ushirikiano wa kiudugu wa Iran uko wazi kwa majirani na nchi zote za eneo.
342/