Bernie Sanders amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, "Ni siku ya huzuni kwa taifa letu kuona Benjamin Netanyahu anaalikwa na viongozi wa mirengo yote miwili ya kisiasa (Marekani) kuihutubia Kongresi."
Ameeleza bayana kuwa, "Netanyahu ni mtenda jinai ya kivita, hastahiki kualikwa kuhutubia kikao cha pamoja cha Kongresi ya Marekani. Bila shaka sitahudhuria (kikao hicho)."
Juzi Ijumaa, viongozi wa Kongresi akiwemo Spika wa Baraza la Mawakilishi wa chama cha Republican, Mike Johnson, kingozi wa bunge hilo wa chama cha Democratic, Hakeem Jeffries, Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Chuck Schumer wa Democratic, na mwenzake wa Wachache, Mitch McConnell wa Republican walimualika Netanyahu kuhutubia kikao cha Kongresi; mwaliko ambao Waziri Mkuu huyo mbabe wa vita ameukubali.
Duru za habari zimeliambia gazeti la The Hill kuwa, Netanyahu yumkini akaihutubia Kongresi katika kipindi cha wiki nane zijazo, au baada ya likizo ya mabunge hayo mnamo Agosti.
Sanders, ambaye ni mwanasiasa wa mrengo wa kushoto wa Marekani amebainisha kuwa, Washington inabeba dhima ya mauaji ya kutisha yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo lililozingirwa la Ukanda wa Gaza.Seneta huyo wa kujitegemea wa Marekani amekuwa akisisitiza kuwa, serikali ya Washington ni mshirika katika jinai za kutisha za Israel huko Ukanda wa Gaza kutokana na uungaji mkono wake kwa utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Wapalestina zaidi ya elfu 36 wameuawa shahidi hadi sasa na wengine zaidi ya elfu 80 wamejeruhiwa katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel huko Gaza.
342/