Mpango wa kuwawekea vikwazo maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ambao wanahusika katika kesi ya uchunguzi dhidi ya viongozi wa Israel uliidhinishwa siku ya Jumanne kwa kura 247 za ndio dhidi ya kura 155 za hapana katika Baraza la Wawakilishi la Marekani Congress ambapo karibu Warepublican wote waliohudhuria kikao hicho walipiga kura ya kuunga mkono na Wanademokrat 42 pia walijiunga na hatua hiyo dhidi ya ICC.
Hata hivyo, mswada huo yamkini usipitishwe katika Baraza la Seneti inayodhibitiwa na Wademokrat, na kwa sababu hiyo, mpango huo unaweza kuonekana kuwa wenye muundo wa nembo ya upinzani wa Marekani dhidi ICC. Michael McCaul, mwenyekiti wa kamati ya mahusiano ya kigeni ya Baraza la Wawakilishi la Marekani ambaye ni wa chama ca Republican ameilaani ICC na kudai kuwa imevuka mipaka kwa kutaka Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa Israel akamatwe.
Vikwazo vilivyowekwa katika muswada huo dhidi ya mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na wanachama wengine wa mahakama hii ni kuwazuia kuingia katika ardhi ya Marekani. Pia, kwa mujibu wa mpango huo, visa za kusafiria za maafisa wa mahakama ya ICC ambao kwa sasa wanaruhusiwa kuingia Marekani zitabatilishwa, na pia watapigwa marufuku kununua nyumba na miamala ya mali isiyohamishika nchini Marekani.Bila shaka, ikiwa mpango huu utapitishwa katika Seneti na kuwa sheria, itamlazimu Rais wa Marekani kuweka vikwazo dhidi ya maafisa wa ICC ambao watahusika katika jaribio lolote la kuchunguza, kukamata, kuweka kizuizini au kumuhukumu mtu yeyote anayeungwa mkono na Marekani na washirika wake.
Wawakilishi wa chama cha Republican katika bunge la Marekani Mei 8 walitangaza kuwa wanatayarisha mpango wa kuiwekea vikwazo ICC iwapo mahakama hii ya Umoja wa Mataifa itatoa kibali cha kukamatwa viongozi wa Israel. Utawala wa Biden ulikuwa umeliita ombi la hati ya kukamatwa Netanyahu na watenda jinai wenzake kuwa eti ni ya 'kidhalimu' lakini haukuunga mkono vikwazo dhidi ya ICC. Joe Biden hapo awali alitangaza "upinzani wake mkubwa" kwa vikwazo hivi dhidi ya ICC na kusema kwamba Ikulu ya White haiviungi mkono.
Hatua hii ya Baraza la Wawakilishi la Marekani imechukuliwa baada ya Karim Khan, mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, kutaka itolewe hati ya kukamatwa Waziri Mkuu na Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel, jambo ambalo limeikasirisha Marekani. Alitangaza katika mkutano na waandishi wa habari kwamba anajaribu kutoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wa Vita wa Israel Yoav Galant kwa kinai za kivita katika Ukanda wa Gaza. Majaji wa mahakama ya ICC wanapasa kutoa uamuzi wao kuhusu ombi la mwendesha mashtaka mkuu huyo. Haijabainika wazi uamuzi huo utachukuliwa lini. Maamuzi haya wakati mwingine huchukua wiki au miezi kadhaa.
Wakati huo huo, serikali ya Biden bado inajaribu kuwahadaa walimwengi kuwa utawala katili wa Israel haujatenda jinai za kivita. Kuhusiana na hilo, Matthew Miller, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, alidai kuwa bado haijabainika iwapo Israel imefanya uhalifu wa kivita huko Gaza baada ya Rais Joe Biden kuiunga mkono Israel katika vita vya Gaza.
Ingawa jinai za utawala wa Kizayuni hususan mauaji ya halaiki ya watu wa Gaza na vile vile utumiaji wa silaha ya njaa dhidi ya Wapalestina ni suala lililo wazi na lisilopingika, lakini Marekani inazuia kulaaniwa utawala huo katili katika taasisi za kimataifa kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Baada ya Afrika Kusini kuishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa kukiuka Mkataba wa Geneva dhidi ya Mauaji ya Kimbari (1948), Ikulu ya White House ilitangaza waziwazi upinzani wake dhidi ya hatua hiyo.
Kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni iliripoti hivi karibuni kwamba kuna uwezekano wa kutiwa mbaroni viongozi wakuu wa Tel Aviv na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Kwa hakika, kuidhinishwa mpango wa vikwazo dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai katika Baraza la Wawakilishi la Marekani ni ishara nyingine ya uungaji mkono wa pande zote wa Washington kwa utawala wa Kizayuni na matumizi mabaya ya madaraka na nafasi yake katika kuadhibu taasisi za kimataifa za mahakama kwa ajili ya kuzuia kufunguliwa mashtaka viongozi wakuu wa Israel wanaotuhumiwa kuhusika na makosa ya jinai. Hakuna shaka kuwa jinai za Kizayuni katika vita vya Gaza hususan mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanatekelezwa kwa amri ya moja kwa moja ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wa Vita Yoav Kalant. Hata hivyo ushahidi usio na shaka katika mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza umezidisha mashinikizo ya kimataifa ya kutolewa hati ya kukamatwa viongozi wakuu wa utawala haramu wa Israel na kufikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Nukta muhimu ni kwamba licha ya vitisho na upinzani wa Marekani kuhusu kukamatwa vinara wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kutoa vitisho dhidi ya mahakama ya ICC ambayo inataka kuwakamata watenda jinai hao, lakini hatua za hivi karibuni za taasisi hizo za mahakama zikiwemo ICC na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhdi ya Israel ni dalili kuwa Marekani inakabiliwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wa vikwazo na vitisho dhidi ya taasisi hizo za kimataifa. Inavyoelekea ni kuwa Marekani itaendelea kutengwa kimatiafa iwapo itatekeleza vitisho vyake hivyo dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya JInai.
342/