BRICS awali ilijumuisha Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini na mwaka huu ilipanuka na kujumuisha Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Idadi ya watu katika nchi za BRICS ni bilioni 3.5 yaani asilimia 45 ya watu wote duniani. Aidha nchi za BRICS zinamiliki asilimia 25 ya biashara ya kimataifa, asilimia 40 ya uzalishaji wa mafuta na asilimia 28 ya Pato Ghafi la Taifa duniani.
Russia na China hufanya karibu asilimia 70 ya mabadilishano yao ya kiuchumi kwa kutumia sarafu za kitaifa; Brazil nayo inaongoza vuguvugu la kuondoa sarafu ya dola katika eneo la Amerika ya Kusini. Afrika Kusini, mwanachama mwingine wa BRICS, inafuatilia kwa karibu mkakati wa kuondoa sarafu ya dola katika mabadilishano ya kibiashara barani Afrika. Aidha Russia na Iran zinatumia sarafu za kidijitali katika biashara ya kimataifa. Saudi Arabia kwa upande wake imeafiki kuuza mafuta yake kwa sarafu isiyo ya dola ya Marekani; Argentina na Brazil zinapanga kuunda sarafu za pamoja, na Brazil na Uchina zimekubali kuacha kutumia dola ya Marekani kama sarafu ya kibiashara baina yao.
Bila shaka, baadhi ya nchi za Ulaya pia zinachukua hatua za kudhoofisha dola ya Marekani. Katika muktadha huu, tunaweza kuashiria kauli za Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu kupunguza utegemezi wa bara la Ulaya kwa "dola ya Marekani' na ombi lake la kutaka bara la Ulaya lialikwe katika mkutano ujao wa BRICS.
Kulingana na takwimu za akiba ya fedha za kigeni zilizochapishwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF), nafasi ya dola ya Marekani katika hifadhi ya fedha kimataifa imepungua kutoka asilimia 66 mwaka 2003 hadi takriban asilimia 58 katika miaka ya hivi karibuni.Alexander Babakov, Naibu Spika wa Bunge la Russia, Duma, akizungumza New Delhi mnamo Machi 2023 alisema kuwa malipo ya kidijitali yanaweza kuwa chaguo bora zaidi katika siku zijazo. Babakov alipendekeza kuwa sarafu ya kidijitali ipewe thamani kwa kutegemea dhahabu na bidhaa nyingine adimu.
Nchi za BRICS sasa zinapanga kuanzisha sarafu mpya ambayo itategemea dhahabu.
Sarafu ya kidijitali ya BRICS inaweza kutumia uwezo wa teknolojia ya blockchain na kutoa suluhisho la hali ya juu kwa akiba ya kidijitali ya fedha katika uga wa kimataifa. Chaguo hili hurahisisha shughuli za mipakani na kuongeza ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi wanachama. Kwa hakika, kuanzishwa kwa sarafu ya BRICS kutakuwa hatua ya ujasiri kuelekea kuondolewa sarafu ya dola ya Marekani ambayo imekuwa ikitegemewa sana katika biashara ya kimataifa.
Nchi za BRICS zinajaribu kuimarisha utawala wao wa kifedha na kujikinga na athari hasi za vikwazo vya Magharibi hasa Marekani kwa kupunguza utegemezi wa dola ya Marekani na kupitisha mbinu mbadala za malipo.
Ripoti mbali mbali zimesisitiza kuhusu kuundwa sarafu itakayosimamiwa na Benki Mpya ya Maendeleo (NDB) iliyoanzishwa na kundi la BRICS.
Kinyume na ilivyo katika Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya BRICS imegawanya hisa zake kwa usawa kati ya nchi tano wanachama waanzilishi.
Kila nchi mwanachama ina haki sawa za kupiga kura na kufanya maamuzi na mchango sawa ulioidhinishwa awali. Muhimu zaidi, hakuna nchi iliyo na kura ya turufu. Benki ya Maendeleo ya Kitaifa ya BRICS ni tofauti na Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia, ambayo hutumia dola ya Marekani kama sarafu kuu kwa shughuli za kimataifa.
Kwa jumla, mambo mawili yameongeza kasi ya uondoaji wa dola katika mabadilishano ya nchi, haswa kati ya wanachama wa BRICS: Moja ni hatua ya Marekani kuzuia akiba ya fedha za kigeni za Russia baada ya vita vya Ukraine mnamo Februari 2022, na pili ni kuongezeka katika nakisi ya bajeti na madeni makubwa ya Marekani, ambayo leo imevuka dola trilioni 30 na hata kulingana na makadirio fulani, impepindukia dola trilioni 50.
342/