6 Julai 2024 - 16:39
Rais wa Marekani alikoroga tena; asema: Naona fahari kuwa mwanamke mweusi

Rais Joe Biden wa Marekani kwa mara nyingine tena ameboronga katika uzungumzaji na kuonyesha udhaifu wa kiakili, baada ya kudai kuwa yeye ni mwanamke mweusi.

Katika mahojiano ya karibuni na idhaa ya WUDU ya Philadelphia, Biden alijikanganya na kusema, "Kama nilivyosema, naona fahari kuwa makamu wa kwanza rais....mwanamke wa kwanza mweusi, kuhudumu na rais mweusi."

Aidha katika mahojiano hayo na Andrea Lawful-Sanders, Biden alivurunda tena kwa kusema, "Mimi ni rais wa kwanza kupigiwa kura na jimbo zima.....jimbo la Delaware, nilipokuwa mtoto."

Kiongozi huyo kizee wa Marekani ni maarufu kwa kuboronga, akionyesha usahaulifu katika uzungumzaji kwa kutoa maelezo yasiyo sahihi na hata katika utembeaji, huku wakosoaji wake wakitoa angalizo kwamba matukio kama hayo yanazidi kuwa ya mara kwa mara kila uchao, na kuyataja kama ushahidi wa kuzorota kwa akili ya mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 81.Alkhamisi iliyopita, Biden katika mdahalo wa urais na Donald Trump alionekana kusitasita na kudumaa mara kwa mara, na pia kuparaganyika kimawazo, jambo lililoibua wasiwasi zaidi kuhusu ukongwe na umri wake mkubwa. Hii ni katika hali ambayo, uchunguzi wa maoni uliofanywa na mtandao wa CBS wa Marekani ambao matokeo yake yalichapishwa Jumapili iliyopita umeonyesha kuwa, takriban robo tatu ya wapiga kura waliojiandikisha nchini Marekani wanaamini kuwa Rais Joe Biden hana afya ya kiakili inayomfanya astahiki kuchaguliwa tena kuongoza nchi katika kipindi cha miaka minne ijayo.

342/