13 Julai 2024 - 15:50
Kitanzi kinazidi kubana koo ya Biden.. Wafadhili waungana na wanasiasa kutaka asigombee urais

Gazeti la New York Times limeripoti kwamba kundi la wafadhili mashuhuri wa chama cha Democratic wameungana na wanasiasa kupinga jaribio la Joe Biden la kutaka kugombea urais wa Marekani kwa muhula wa pili katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba ijayo.

Gazeti hilo limesema kuwa, kundi la wafadhili limeifahamisha kamati kubwa zaidi ya kisiasa inayomuunga mkono Biden kwamba takriban dola milioni 90 za michango zitasimamishwa iwapo Rais Biden atang'ang'ania kugombea urais katika uchaguzi ujao.

Awali, wanasiasa kutoka chama cha Democratic walipinga fikra ya kugombea Biden katika uchaguzi huo kutokana na umri wake mkubwa na utendaji duni katika mdahalo aliofanya Juni mwaka huu kati yake na mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump.

Gazeti la Washington Post limemnukuu Seneta Mdemokrati, Peter Welch akisema: "Kwa ajili ya nchi, natoa wito kwa Rais Biden kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais."

Hadi sasa, wawakilishi 17 wa chama cha Democratic wametangaza kupinga ugombea wa Biden, mwenye umri wa miaka 81, katika uchaguzi ujao wa rais.Matokeo ya kura ya maoni iliyofanywa na ABC, Washington Post, na Ipsos yameonyesha kuwa 67% ya Wamarekani, wakiwemo wafuasi wa Biden, wamesema kwamba anapaswa kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais, baada ya utendaji wake dhaifu katika mdahalo na mpinzani wake wa Republican, Donald Trump, wiki mbili zilizopita.

342/