20 Julai 2024 - 15:55
Biden anakaribia kujiondoa, wagombea 4 wanajitayarisha kumrithi

Rais wa Marekani, Joe Biden, anakaribia kufanya uamuzi wa kujiondoa katika kinyang'anyiro cha kuwania tena kiti cha urais katika uchaguzi ujao. Haya ni kwa mujibu wa wa habari zilizovuja zinazothibitisha kwamba, chama cha Democratic kwa sasa kinajadili machaguo ya hatua zinazofuata.

Duru za habari zinasema kwamba, majadiliano ya awali ndani ya chama cha Democratic yanapendekeza kwamba, Rais Joe Biden ataitisha ushindani wa wazi wa kuwania nafasi ya kukiwakisha chama hicho kwenye uchaguzi wa mwishoni mwa mwaka huu katika mkutano ujao wa chama.

Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa, majadiliano ya baadhi ya Wademokrati yanasukuma mbele wagombea 3 pamoja na Makamu wa Rais, Kamala Harris, akiwemo Gavana wa California, Gavin Newsom.

Gazeti la New York Times limemnukuu mtu wa karibu wa Biden akisema kuwa, ingawa Rais wa Marekani bado hajachukua uamuzi wa kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais, haitashangaza iwapo atatangaza hivi karibuni kumuunga mkono Kamala Harris kama mgombea mbadala.

Kwa upande wake, gazeti la Washington Post, limewanukuu maafisa 3 wa Chama cha Democratic kwamba spika wa zamani wa bunge, Nancy Pelosi amewafahamisha baadhi ya Wademokrati katika bunge hilo kwamba anaamini Rais Joe Biden anaweza kushawishiwa kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais.

Gazeti hilo limeripoti kuwa Pelosi anaamini kwamba Biden anakaribia kuchukua uamuzi wa kuachana na azma yake ya kugombea tena kiti cha rais wa nchi hiyo.Biden, mwenye umri wa miaka 81, anakabiliwa na mashinikizo makubwa kutoka kwa viongozi mashuhuri wa chama cha Democratic wanaomtaka ajiondoe kwenye uchaguzi ujao wa rais baada ya kutofanya vizuri katika mdahalo dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Republican, rais wa zamani Donald Trump, ambao uliibua wasiwasi kuhusu umri wake na uwezo wa kushinda uchaguzi wa Novemba.


342/