Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Haj Abul Alaa al-Walaiy, Katibu Mkuu wa Kataib Sayyid al-Shuhadaa, amesema kuwa Hashd al-Shaabi ni nguzo kuu ya Taifa la Iraq na kwamba Muqawama (Upinzani) ni heshima ya Umma wa Taifa la Iraq ambayo daima itaendelea kuhitajika.
Akizungumza katika hafla ya kumbukumbu ya siku arobaini tangu kuuawa shahidi kwa kamanda Sayyid Haidar Mousawi, al-Walaiy alieleza kwa huzuni kwamba: “Siku arobaini hizi zilikuwa nzito kwetu kama miaka arobaini – zenye huzuni na maumivu. Ndugu yangu, msaidizi wangu, na mwenye kuhifadhi siri zangu!” Alitaja pia kwamba kuingiliana kwa kumbukumbu hiyo na matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) ni neema ya Mwenyezi Mungu inayofufua bustani ya jihadi upya.
Shahidi Mousawi: Mshipa Hai wa Kataib Sayyid al-Shuhadaa na Mtetezi wa Haram
Al-Walaiy alimtaja shahidi Mousawi kuwa ni kamanda thabiti, mkweli na aliyetoa roho yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, akisema: “Maisha na juhudi zake haziwezi kueleweka kwa khutba au kitabu chochote.” Alimwelezea kama mshipa hai wa kundi la Kataib Sayyid al-Shuhadaa na aliyekuwa mstari wa mbele katika kutetea Haram ya Sayyida Zaynab (as).
Aidha, alikumbusha kuwa shahidi Mousawi alikuwa miongoni mwa wa kwanza kuchukua silaha dhidi ya Daesh, akielekea vitani kutetea taifa. Katika vita vya Tofaan al-Aqsa, aliibuka kuwa mpiganaji mwenye ushawishi mkubwa katika mhimili wa Muqawama. Al-Walaiy aliongeza: “Hakuna kitu kilichoweza kumzuia kutekeleza jukumu lake la Kiungu. Alimpenda Ali (as) na Hussein (as), na aliendeleza njia ya mashahidi wa Quds.”
Damu ya Mashahidi: Kizuizi Dhidi ya Adui
Al-Walaiy alisisitiza kuwa damu ya mashahidi wa Iraq imekuwa ngome dhidi ya kuenea kwa utawala wa Kizayuni. “Kama si damu yako na ndugu zako mashahidi, leo hii Israel ingekuwa imefika hadi mipaka ya Baghdad, kama ilivyo leo katika mipaka ya Damascus.” Alisema damu hiyo safi imezuia kurudiwa kwa janga la Gaza na kulinda miji ya Iraq dhidi ya kuangukia mikononi mwa maadui.
Aidha, alikanusha madai ya baadhi ya maadui kwamba silaha za Hashd na Muqawama ni tishio kwa serikali, akisema: “Wakati theluthi moja ya Iraq ilidhibitiwa na Daesh, ni wapiganaji wa Hashd na Muqawama waliobadilisha hali ya vita na kuokoa Iraq, raia wake, na mustakabali wake.”
Muqawama: Nguzo ya Iraq na Heshima ya Umma
Katika hitimisho la hotuba yake, Haj Abul Alaa al-Walaiy alitaja nafasi muhimu ya Muqawama katika Iraq na ukanda mzima wa Mashariki ya Kati. Alisema: “Adui Mmarekani na Mzayuni wanafahamu vyema kuliko wengine ndani ya Iraq kwamba kuwepo kwa Hashd na Muqawama ni kizuizi kikubwa dhidi ya mradi wao wa ‘Mashariki ya Kati Mpya’.”
Alieleza kuwa utiifu kwa Marjaa’iyya (uongozi wa kidini) ndio dhamana ya usalama wa Iraq: “Tunatii Marjaa’iyya na tunaiheshimu, kwani ndiye mdhamini wa amani ya nchi yetu.” Alisisitiza kuwa Hashd ni nguzo ya Iraq, na Muqawama ni heshima ya Umma ambayo haiwezi kupuuzwa.
Akihitimisha, alikataa kwa msimamo mkali mawazo ya upatanisho na wavamizi au uhusiano wa kawaida nao, akisema: “Silaha ya Muqawama ni alama ya heshima na utukufu wetu.”
Pia alisisitiza mshikamano na watu wa Gaza: “Tunaweka Gaza hai ndani ya nyoyo zetu na tuko tayari daima kuwasaidia.” Alieleza kuwa ushindi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni furaha kwao, na kwamba ndugu zao wa Lebanon ni mfano wa ushindi - ushindi uliotabiriwa na Qur’ani Tukufu.
Your Comment