2 Agosti 2025 - 17:53
Source: Parstoday
Jeshi la Yemen lashambulia ngome 3 za Israel kwa kutumia droni 5

Jeshi la Yemen limetangaza kuwa limetekeleza mashambulizi matatu ya ndege zisizo na rubani (droni) katika maeneo matatu ya Israel.

Televisheni ya al Masira imetangaza kuwa, taarifa ya jeshi la Yemen iliyosomwa na msemaji wa jeshi hilo, Brigedia Jenerali Yahya Saree imesema katika shambulio la kwanza, droni mbili za Yemen zimelenga shabaha muhimu ya utawala wa Kizayuni. Katika shambulio la pili, droni mbili zimepiga kituo cha kijeshi huko Askalan, na katika oparesheni ya tatu, droni moja ya Yemen imepiga shabaha ya kijeshi katika eneo la Negev.  

Jeshi la Yemen limetangaza kuwa oparesheni zote tatu zimetekelezwa kwa mafanikio. Katika taarifa yake hiyo, jeshi la Yemen limetoa wito kwa raia wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kutekeleza wajibu wao ili kuwahami wenzao wa Palestina na kulaani jinai za Wazayuni kwa kufanya maandamano kwa wingi katika siku zijazo. 

Jeshi la Yemen limetahadharisha pia kuwa, litaendelea kuushambulia utawala wa Kizayuni hadi hapo Israel itakapositisha mashambulizi yake dhidi ya watu wa Gaza na kuondoa mzingiro katika eneo hilo. 

Jeshi la Yemen limetekeleza mashambulizi haya dhidi ya Israel masaa machache baada ya utawala wa Kizayuni kudai kuwa umesambaratisha mashambulizi hayo. 

Your Comment

You are replying to: .
captcha