21 Julai 2024 - 15:48
EU yaunga mkono uamuzi wa ICJ kuhusu uvamizi haramu wa Israel huko Palestina

Mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa imeamua kwamba ukaliaji wa mabavu wa miaka 57 wa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina ni kinyume cha sheria, uamuzi ambao Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, amesema unakaribiana na misimamo ya Umoja wa Ulaya (EU).

Josep Borrell amesema kwamba; EU imefanya "zingatio zuri" la uamuzi wa mahakama hiyo na kutaka misimamo yake iungwe mkono kimataifa.

Amesema: "Katika ulimwengu ambao sheria za kimataifa zinakiukwa mara kwa mara, ni wajibu wetu wa kimaadili kuthibitisha dhamira yetu isiyoyumba kwa maamuzi yote ya ICJ kwa njia thabiti na bila kujali mada husika."Josep Borrell ameongeza kwamba uamuzi wa mahakama ya ICJ itabidi uchambuliwe kwa kina zaidi, ikiwa ni pamoja na athari zake kwa sera za EU.

Siku ya Ijumaa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilisema kwamba; "kuendelea kuwepo utawala ghasibu wa Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria", na kuongeza kuwa utawala huo "unakiuka sheria kwa kuendeleza mashambulio ya kinyama katika Ukanda wa Gaza na kuutaka ukomeshe "haraka iwezekanavyo" mashambulizi hayo yasiyo ya kibinadamu dhidi ya watu madhulumu wanaozingirwa huko Gaza.

Utawala ghasibu wa Israel ulivamia na kukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na al-Quds Tukufu Mashariki, maeneo ambayo Wapalestina wanayataka kwa ajili ya kuunda taifa lao huru la baadaye, katika vita vya mwaka 1967.

Uamuzi huo unayahimiza mataifa yote na mashirika ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa, (UN) "kutotambua kuwa halali" hali inayotokana na kuwepo kinyume cha sheria kwa utawala wa Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo wa kizayuni.


342/