22 Julai 2024 - 16:30
Republican: Biden ni punguani, asiachiwe kitufe cha silaha za nyuklia

Muda mfupi baada ya Rais Joe Biden wa Marekani kutangaza kujiondoa katika kinyang'anyiro cha kutetea kiti chake cha urais, viongozi waandamizi wa chama cha Republican wamesema mwanasiasa huyo mwenye miaka 81 hapasi kuachiwa nywila (kodi) za kitufe cha silaha za nyuklia kutokana na matatizo ya kisaikolojia yanayomsumbua.

Mjumbe wa North Carolina, Richard Hudson, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kongresi ya chama cha Republican amesema: Hili ni sakata la kihistoria. Rais Biden hana uwezo wa kuendelea kuongoza, Wanademocrat walijua, na waliwaongopea Wamarekani ili kuficha (mambo). Ikiwa Biden hafai kufanya kampeni kutokanan na matatizo ya kiakili , hafai pia kuwa na nywila za nyuklia.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani, Mike Johnson ambaye amesema: "Ikiwa Joe Biden hafai kuwania urais, hafai kuendelea kuhudumu kama rais. Ni lazima ajiuzulu mara moja. Novemba 5 (tarehe ya uchaguzi) ipo mbali sana."

Wabunge wengi wa chama cha Republican wamejiunga na wimbo huo wa kumtaka Biden ajiuzulu. Seneta wa Florida, Rick Scott, Mwakilishi wa Louisiana, Steve Scalise, na Mwenyekiti wa Baraza la Republican bungeni, Elise Stefanik wa New York ni miongoni mwa makumi ya wanasiasa ambao wanamshinikiza Biden ajiuzulu urais mara moja.Biden amelazimika kujitoa katika mbio za kutetea kiti chake cha urais baada ya kuongezeka mashinikizo ya kumtaka ajiondoe kutokana na sababu mbalimbali likiwemo suala la afya na uwezo wake wa kukumbuka mambo. Baada ya kuthibitisha kuwa anajiondoa katika kinyang'anyiro cha urais, Biden alimuidhinisha Makamu wa Rais Kamala Harris kuchukua nafasi yake.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa karibuni na mtandao wa CBS wa Marekani umeonyesha kuwa, takriban robo tatu ya wapiga kura waliojiandikisha nchini Marekani wanaamini kuwa Rais Joe Biden hana afya ya kiakili inayomfanya astahiki kuchaguliwa tena kuongoza nchi katika kipindi cha miaka minne ijayo.


342/