26 Julai 2024 - 17:11
Katibu Mkuu wa UN: Watu nusu milioni wanakufa kila mwaka kwa joto kali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa dharura wa kuchukuliwa hatua ili kulinda vyema mabilioni ya watu duniani kote walioathiriwa na athari za joto kali, huku ongezeko la joto duniani likiendelea kupanda bila ya kuwepo dalili ya kupungua.

Guterres ametoa wito huo katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na akatoa indhari kwa kusema: "mabilioni ya watu wanakabiliwa na janga la joto kali linalotokana na mawimbi ya joto yanayozidi kukatili maisha huku halijoto ikizidi nyuzi joto 50 kote ulimwenguni. Hiyo ni nyuzi joto 122 Fahrenheit ikiwa ni nusu ya kiwango cha kuchemka”.

Katibu Mkuu wa UN ameendelea kusema: "Ujumbe uko bayana, joto linapanda. Joto kali lina athari kubwa kwa watu na sayari. Ulimwengu lazima ukabiliane na changamoto ya kupanda kwa halijoto.”

Kwa mujibu wa Gutterres, joto linakadiriwa kuua karibu watu nusu milioni kwa mwaka, ikiwa ni takribani mara 30 zaidi ya vifo vinavyosababishwa na vimbunga vya kitropiki.

342/