30 Julai 2024 - 19:36
Ujumbe wa pongezi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Rais Masoud Pezeshkian

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa kupongeza kuchaguliwa Rais Masoud Pezeshkian kuwa rais mpya wa Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran ametangaza utayarifu wa shirika hilo la kimataifa kwa ajili ya kushirikiana na serikali mpya ya Iran.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake akielezea furaha yake kutokana na kuchaguliwa kwa Masoud Pezeshkian  kuwa rais mpya wa Iran, amesema kuwa Umoja wa Mataifa unatarajia kufanya kazi pamoja na serikali mpya ya Iran.
Aidha katika kumtakia mafanikio Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Daktari Masoud Pezeshkian, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameashiria nafasi muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu katika eneo na kusema; Kutekeleza jukumu la serikali mpya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kusaidia kutatua migogoro ya kikanda na kuzuia migogoro mipya kunaweza kuwa na umuhimu mkubwa katika kuimarisha usalama wa kikanda na wa nje ya kanda. Guterres pia amesisitiza kuwa dhamira ya Umoja wa Mataifa ni kuendelea kuunga mkono juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu. Katika duru ya pili ya uchaguzi wa awamu ya 14 ya rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, uliofanyika siku ya Ijumaa, tarehe 5 Julai, mwaka huu, Masoud Pezeshkian alichaguliwa na wananchi kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Alipata zaidi ya kura milioni 16, na hivyo kuwa rais wa awamu ya 14 wa watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

342/