20 Februari 2025 - 19:58
Oxfam: Tunaanza kuelewa kina cha uharibifu uliofanyika Gaza

Shirika la Oxfam la Uingereza limetangaza kuwa utawala wa Israel umeharibu zaidi ya asilimia 80 ya mitandao ya maji na maji taka ya Gaza na kusababisha hali mbaya ya kiafya.

Taarifa iliyotolewa na Clemence Laguarda, mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Oxfam huko Gaza, imesema: "Sasa, baada milipuko ya mabomu kukoma, ndio kwanza tunaanza kuelewa kina cha uharibifu huo mkubwa."

Oxfam imetangaza kuwa utawala wa Israel umeharibu kilomita 1,650 za mitandao ya maji na maji taka ya Ukanda wa Gaza.

Shirika hilo la misaada ya kibinadamu limesema kuwa wakazi wa kaskazini mwa Gaza na mji wa Rafah kusini mwa eneo hilo, wanapata lita 5.7 tu za maji kwa siku, kiwango ambacho ni chini ya asilimia 7 ya kiasi cha kabla ya vita. Kiasi hiki hakitoshi hata kujisafishia chooni mara moja.

Shirika la Oxfam limeeleza matumaini kuwa usitishaji mapigano utaendelea na kwamba mafuta na misaada ya kibinadamu itafika Gaza ili Wapalestina waweze kujenga upya maisha yao. 

Tathmini ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, na Benki ya Dunia inaonyesha kuwa ujenzi mpya wa eneo la Gaza na Ukingo wa Magharibi unahitaji dola bilioni 53.2 katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

342/