Katika mkutano wake na Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina, Ziyad al-Nakhalah, uliofanyika jana Alkhamisi hapa mjini Tehran, Kamanda wa IRGC ameupongeza Muqawama na mapambano ya Palestina na wakazi wa Gaza kwa ushindi wao dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Meja Jenerali Hossein Salami amesema kuwa, Mhimili wa Muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia upo katika kilele cha nguvu zake, na ndiposa uliwapigisha magoti Mzayuni na waitifaki wake huko Gaza.
Kamanda huyo wa SEPAH ameleza bayana kuwa, utawala haramu wa Israel na Marekani bila ya shaka hatimaye watapata kushindwa, ingawaje wanaweza kupata ushindi wa aina fulani.
"Utawala wa Kizayuni na Marekani ziko katika mkondo wa kushindwa na kuporomoka," Jenerali Salami amesema na kuongeza, "Ushindi wa kimkakati unaweza kucheleweshwa, lakini hakutakuwa na ushindi wa kistratejia (kwa Marekani na Israel)."
Amesema matukio ya Gaza, Yemen na Lebanon yanaashiria ukweli kuhusu utawala wa Kizayuni na kushindwa kwa Marekani. Meja Jenerali Salami amesema, matukio ya hivi karibuni yameonyesha kuwa damu imepata ushindi dhidi ya upanga na wananchi wa Palestina wameibuka na ushindi katika vita dhidi ya Wazayuni.
Kamanda Salami amebainisha kuwa, utawala wa Israel hauwezi kuwepo bila kuungwa mkono na Marekani, na kusisitiza kwamba, “Marekani yenyewe inazidi kudidimia. Hii ndiyo hali halisi inayoshuhudiwa, ikiwa ni sehemu ya mustakabali.”
342/
