21 Februari 2025 - 18:04
Netanyahu adai mabaki ya mwili yaliyorejeshwa si ya Shiri Bibas, HAMAS yamjibu

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amedai kuwa harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imekiuka masharti ya makubaliano ya kubadilishana mateka kwa sababu imekabidhi mwili wa mwanamke asiyejulikana kutoka Ghaza badala ya ule wa mateka wa Kizayuni Shiri Bibas.

Katika taarifa aliyotoa leo, Netanyahu ameapa kwamba Hamas "italipia kwa gharama kubwa" kwa kile alichokiita "ukiukaji mkubwa" wa makubaliano ya kubadilishana mateka.

Mapema leo, jeshi la utawala wa Kizayuni lilidai kuwa maiti liliyopokea kutoka kwa Hamas siku ya Alkhamisi haikuwa ya Bibas, mateka Muisrael ambaye alikuwa akishikiliwa na Muqawama wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza.

Hamas ilitangaza kuwa imekabidhi miili ya Bibas na watoto wake wawili, Ariel na Kfir, pamoja na Oded Lifshitz siku ya Alkhamisi chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano Ghaza na kubadilishana mateka wa Kizayuni na Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala ghasibu wa Israel.

Kufuatia madai yaliyotolewa na Netanyahu, harakati ya Hamas imesema, inaonekana kuwa mwili wa mateka huyo Muisrael utakuwa umechanganywa na mabaki ya watu wengine kutoka kwenye kifusi baada ya shambulio la anga la jeshi la utawala wa Kizayuni kupiga mahali alipokuwa akishikiliwa.

Katika taarifa yake, harakati hiyo ya Muqawama wa Palestina imeeleza kwamba, mateka hao wa Israel waliuawa katika mashambulizi ya kiholela ya anga yaliyofanywa na jeshi la Kizayuni wakati wa vita vya mauaji ya kimbari vya miezi 15 dhidi ya eneo hilo lililowekewa mzingiro.../

342/