21 Februari 2025 - 18:05
Kwa nini nchi za Ulaya zitashindwa tu katika kamari na Trump

Kikao cha viongozi wa nchi kadhaa za Ulaya ambacho kilifanyika hivi karibuni huko Paris kuhusu mgogoro wa Ukraine kilimalizika bila natija yoyote.

Viongozi wa Ujerumani, Uingereza, Italia, Poland, Uhispania, Uholanzi, Denmark, na vile vile Antonio Costa na Ursula von der Leyen, wakuu wa Baraza la Ulaya na Kamisheni ya Ulaya, pamoja na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte walihudhuria kikao hicho. Donald Tusk Waziri Mkuu wa Poland alisema baada ya mkutano huo kwamba, "viongozi wa Ulaya wameshindwa kufanya maamuzi ya pamoja kuhusu suala la Ukraine na hatua za Trump kuhusu mazungumzo ya amani, likiwemo suala la kutuma askari wa kulinda amani nchini Ukraine wakati wa utekelezaji wa makubaliano ya amani yanayotarajiwa."

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitumai kuwa sauti ya umoja ingedhihiri katika kikao cha Paris dhidi ya kutengwa Ulaya katika mazungumzo ya Russia na Marekani huko Riyadh, Saudi Arabia. Suala hilo limethibitisha wazi namna kuna tofauti kubwa za kisiasa na kiusalama kati ya serikali kubwa za Ulaya.

Radiamali ya serikali za Ulaya kwa mpango wa Trump wa kumaliza haraka vita vya Ukraine inaonyesha wazi kwamba hazina mpango wowote wa mapema wa kufanya mazungumzo na Putin. Jeshi la Ukraine halina msukumo wa kuendelea na vita katika hali ambayo serikali ya Kyiv inaziomba serikali za Ulaya ziendelee kuipa misaada zaidi ya kifedha na kijeshi. Wakati huo huo, serikali za Ulaya hazina uwezo wa ziada wa kuongeza msaada wa kifedha na kijeshi kwa Ukraine kwa sababu zinaitegemea sana Marekani kwa ajili ya kuendeleza vita nchini Ukraine.

Kabla ya Trump kurejea Ikulu ya White House, serikali za Ulaya zilitumai kwamba kwa kutegemea msaada wa kijeshi na kifedha wa Marekani kwa Ukraine, zingeweza kuwalazimisha Warussia waketi kwenye meza ya mazungumzo baada ya kupata kipigo kikali cha kijeshi. Lakini kurejea kwa Trump White House kumevuruga kabisa matarajio ya viongozi wa Ulaya kuhusu vita vya Ukraine. Trump ametumia mkanganyiko wa serikali za Ulaya kuhusu jinsi ya kukabiliana na vita vya Ukraine katika kuifedhehesha Ulaya ambapo hata amezinyima fursa ya kushiriki katika mazungumzo na Russia.Jambo la kuzingatia ni kwamba Russia pia imetumia vizuri na kwa maslahi yake msimamo huo wa Trump na kuzifedhehesha zaidi serikali za Ulaya kwa kuziambia kuwa hazifai kushiriki kwenye mazungumzo yoyote ya kumaliza vita nchini Ukraine. Vassily Nebenzia, Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, amesema kuwa Uingereza na Umoja wa Ulaya haziwezi kuwa sehemu ya mazungumzo ya amani ya Ukraine kwa sababu hazina uwezo wa kufanya mazungumzo. Yury Ushakov, mshauri mkuu wa sera za kigeni wa Putin, amethibitisha kuwa mazungumzo na Wamarekani hayatajumuisha upande wa tatu.

Kivitendo, si Ulaya wala serikali ya Ukraine zina nafasi katika mchakato wa mazungumzo na Russia. Moja ya mapendekezo ya Marekani kwa ajili ya kumaliza vita nchini Ukraine ni kwa nchi hiyo ya Ulaya isahau kabisa kukomboa ardhi yake iliyochukuliwa na Russia baada ya 2014. Kifungu kingine cha mpango wa amani wa serikali ya Marekani ni Ukraine kutokuwa mwanachama wa mkataba wa NATO. Misingi hii miwili ni moja ya masharti muhimu yaliyotolewa na Putin kwa ajili ya kusitisha vita na kupatikana amani nchini Ukraine. Serikali za Ulaya hazina hata mpango wa pamoja kwa ajili ya Ukraine baada ya kumalizika vita. Zinajua vizuri kwamba hazina mbadala wa mpango wa Trump wa kumaliza haraka vita nchini humo.

Katika mkutano wa Paris, viongozi wa Ulaya walizungumza kwa muda wa saa tatu na nusu kuhusu kipindi cha baada ya kusitishwa mapigano huko Ukraine na kuundwa jeshi la Umoja wa Ulaya la kulinda amani na kuanzishwa njia mpya za mpaka na Russia katika eneo la Ukraine. Lakini mazungumzo hayo hayakuwa na matokeo yoyote. Ufaransa na Uingereza zilitetea mpango huo lakini Kansela Olaf Schultz wa Ujerumani akasema kuwa yuko tayari kutuma askari wa Ujerumani nchini Ukraine iwapo tu wanajeshi wa Marekani watakuwepo. Wakati huo huo, Pete Hegseth, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alisema katika Mkutano wa Usalama wa Munich kwamba Pentagon haitatuma askari wowote Ukraine kama sehemu ya dhamana ya usalama. Aliongeza kuwa iwapo vikosi vya kulinda amani vitatumwa huko, havitalindwa chini ya utaratibu wa ulinzi wa pamoja wa NATO.

"Hatutarajii kutuma wanajeshi wa Poland nchini Ukraine." Hayo yalisemwa na Donald Tusk, Waziri Mkuu wa Poland katika taarifa yake mjini Warsaw kabla ya kuelekea Paris. Russia pia imetumia tofauti hizo kati ya wanachama wa Umoja wa Ulaya na Ulaya na Marekani kutangaza upinzani wake mkali dhidi ya kutumwa askari wa kulinda amani wa Ulaya katika safu za mapigano ya jeshi la Ukraine na Russia.

Imesema kuwa ni Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pekee ndilo linastahili kutuma wanajeshi wa kulinda amani nchini Ukraine. Serikali za Ulaya zilikuwa hazijawahi kukabiliwa na mzozo na tofauti kama hizo tangu kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Bila shaka vita vya Ukraine na namna ya kuvimaliza kunaashiria kushindwa kukubwa kwa bara la Ulaya baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia.


342/