22 Februari 2025 - 19:34
Mwana wa Nasrullah asema siku ya Jumapili ya mazishi ya baba yake ni "Siku ya Kutangaza Msimamo"

Sayyid Muhammad Mahdi Nasrullah, mwana wa Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon aliyeuawa shahidi amesema katika hotuba ya kuwatolea mwito watu kuhudhuria mazishi ya baba yake kwamba: "kushiriki katika mazishi ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah kutakuwa ni kushiriki mtu katika siku ya kutangaza msimamo na kudhihirisha kivitendo mapenzi yake kwa Shahidi Nasrullah".

Katika wito huo aliotoa kwa njia ya video, Sayyid Mahdi Nasrullah amewataka wale wote wanaompenda kwa dhati Sayyid Hassan Nasrullah kuhudhuria mazishi ya shakhsia huyo adhimu yatakayofanyika kesho Jumapili.

Mwana huyo wa Shahidi Nasrullah amesema: "maadui, wapinzani, na wanaotutakia mabaya walijaribu kufanya kila wawezalo kuzuia shughuli ya mazishi isiweze kufanyika kwa namna yoyote ile."

Sayyid Mahdi ameongezea kwa kusema: "kitu kidogo kabisa ninachoweza kusema kuwaambia wale wote wanaotaka kuhudhuria mazishi siku ya Jumapili ni kwamba 'nyinyi ni waaminifu na watu wenye muamana' ".

Mwana huyo wa kiume wa Katibu Mkuu wa Hizbullah aliyeuliwa shahidi, amebainisha kwa kusema: "amma kwa wale watu ambao wanaweza kuhudhuria, lakini wakaamua wasihudhurie kwa visingizio mbalimbali, kama vya kufurika umati wa watu, mvua, na hata kwa kusema 'mazishi hayatasitishwa kwa kutoshiriki mimi'; wao ninawaambia, Sharifu huyu alisimama imara miaka na miaka kuzikabili dhoruba kali, na akasimama imara kuhimili mvua ya maelfu ya tani za miripuko kwa ajili yenu. Kuhudhuria kwenu siku ya Jumapili si kushiriki katika mazishi tu, lakini pia ni 'Kutangaza Msimamo' ".

Katika ujumbe wake huo, Mahdi Nasrullah ameendelea kueleza: "Jumapili ni siku ya kutangaza upya baia' na ahadi ya 'Tumekuitika Ewe Nasrullah'. Kila yule ambaye alikuwa akisema, "najitolea mhanga maisha yangu, familia yangu, na watoto wangu kwa ajili yako", inapasa siku ya Jumapili adhihirishe mapenzi hayo, nasi sote tutaliona hilo Jumapili".

 Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, miili ya Mashahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah ya Lebanon, na naibu wake Sayyid Hashim Safiyyuddin, imepangwa kuzikwa kusini mwa Lebanon kesho Jumapili Februari 23, 2025. 

Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, ambaye alihudumu kama Katibu Mkuu wa Hizbullah kwa zaidi ya miaka 30, aliuawa shahidi siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Septemba katika shambulio la kigaidi la anga lililofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika eneo la viunga vya kusini mwa Beirut.

Naye Shahidi Hashem Safiyyuddin, Mkuu wa Baraza la Kisiasa la harakati hiyo ya Muqawama aliuawa shahidi katika shambulio jengine la kigaidi lililofanywa na Israel karibu wiki moja baada ya kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah.../

342/