22 Februari 2025 - 19:37
Iran yaendelea kumiliki ujuzi wa ujenzi wa Mitambo ya Nyuklia

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema kuwa Marekani imeshindwa kuzuia ujenzi wa mtambo wa nyuklia wa Karun katika jiji la Darkhovein, kusini magharibi mwa Iran, akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kufuatilia shughuli zake za nyuklia kwa amani licha ya njama za maadui.

Mohammad Eslami alisema: "Ulimwengu mzima unajua kuwa Iran inaendelea kupata maarifa ya kujenga mitambo ya nyuklia."

Alitoa matamshi hayo wakati wa hafla iliyofanyika katika eneo la ujenzi wa mtambo wa umeme wa nyuklia wa Karun, uliopo katika Wilaya ya Darkhovein, Kaunti ya Shadegan, mkoa wa Khuzestan.

Aliongeza kuwa: "Ili kufanikisha malengo yetu, hatujali vikwazo na shinikizo kutoka kwa maadui." Pia alibainisha kuwa: "Tutaendelea na njia tuliyojiwekea ili kufanikisha malengo yetu."

Akitaja nafasi ya Iran katika nyanja ya ujuzi wa ujenzi wa mitambo ya nyuklia, Eslami alisema: "Iran imekuwa mhusika mkuu katika maarifa ya kujenga mitambo ya nyuklia duniani, na maadui hawawezi kuvumilia mafanikio haya makubwa."

Akitilia mkazo umuhimu wa ujuzi huu katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tiba na kilimo, Eslami alisisitiza kuwa maadui hawawezi kuizuia Jamhuri ya Kiislamu kufanikisha malengo yake kwa kuwaua wanasayansi wake au kwa kuweka vikwazo na shinikizo la kiuchumi dhidi ya nchi.

Akizungumzia ujenzi wa mtambo wa nyuklia wa Karun wenye uwezo wa megawati 300, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema kuwa operesheni hiyo "inaendelea vizuri."

Akitilia mkazo kwamba Iran inaendelea na shughuli zake za nyuklia kwa amani licha ya mashinikizo, Eslami amesema: "Miaka kumi na miwili iliyopita, Marekani ilijaribu kusimamisha mchakato wa ujenzi wa mtambo wa nyuklia wa Darkhovein lakini imeshindwa."

Kulingana na ripoti, mtambo huo wa nyuklia ni wa aina ya kinu cha nyuklia cha maji yenye shinikizo kubwa (Pressurized Water Reactor - PWR) na una uwezo wa kuzalisha megawati 300 za umeme. Mtambo huu unatarajiwa kujengwa kwenye eneo la takriban hekta 50 karibu na Mto Karun.

342/