Akizungumza siku ya Jumatano, Februari 19, katika kikao cha "Ubunifu wa Uwekezaji wa Baadaye" huko Miami, Florida, Trump alidai kwamba kunapaswa kuwa na utulivu na amani katika Mashariki ya Kati, na kwa sababu hiyo, ameanzisha tena sera ya mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran ili kuleta amani katika eneo na wakati huo huo kuliweka kundi la Ansarullah la Yemen katika orodha ya makundi yanayodaiwa kuwa ya kigaidi.
Trump pia alidai mnamo Februari 4, 2025, wakati wa kutia saini hati ya utendaji ya kuendeleza sera ya mashinikizo ya juu dhidi ya Iran, kwamba yuko tayari kuzungumza na rais wa Iran. Alisema: "Tuna haki ya kusimamisha uuzaji mafuta ya Iran kwa nchi nyingine". Trump, ambaye alitekeleza sera hiyo iliyofeli dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika muhula wa kwanza wa urais wake, kwa mara nyingine tena katika utawala wake wa pili, amedai kwamba anatumai hakutakuwepo na haja ya kutumia chaguo hilo la mashinikizo ya juu zaidi, iwapo Marekani itafikia makubaliano na Iran.
Kwa miaka mingi, Marekani imekuwa ikiituhumu Iran kuwa ina mpango wa kijeshi wa kutengeneza silaha za nyuklia bila kutoa ushahidi wowote na imechukua hatua kubwa za kisiasa na kutekeleza vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran kwa kisingizio hicho. Katika muhula wa kwanza wa urais wake, Trump na Joe Biden, Rais aliyeondoka madarakani wa chama cha Democratic, mara kwa mara walitoa madai ya Iran kuwa na mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia na kusisitiza juu ya kuizuia kupata silaha hizo. Sasa, akiwa mwanzoni mwa muhula wake wa pili wa urais, Trump anakariri madai hayo hayo yasiyo na msingi na kutumia kisingizio hicho kuanzisha tena mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran. Katika muhula wake wa kwanza wa urais, Trump alijitoa katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA ili kuuridhisha utawala ghasibu wa Israel na kufikia malengo yake binafsi dhidi ya Iran. Alidai kuwa mapatano hayo ya JCPOA yalikuwa mapatano mabaya zaidi kuwahi kusainiwa na Washington. Kisha mnamo tarehe 8 Mei 2018, na baada ya kutangaza kuitoa Marekani katika mapatano ya JCPOA, aliyaweka pembeni mapatano hayo na kukataa kutekeleza majukumu yake chini ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa licha ya upinzani mkubwa wa kimataifa.Ili kuilazimisha Iran ikubali matakwa yake haramu, utawala wa Trump ulitekeleza vikwazo visivyo na mfano wake katika fremu ya kampeni ya mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Tehran na kupinga mpango wowote wa kutekelezwa JCPOA. Utawala wa Trump umerejesha orodha ndefu ya vikwazo vya kiuchumi ambavyo viliondolewa chini ya makubaliano hayo ili kuilazimisha Iran ikubali matakwa yake. Ikulu ya White House iliendelea kuweka vikwazo vipya karibu 1,500 dhidi ya Iran katika juhudi zake za kujaribu kuiburuza Tehran kwenye mazungumzo mapya. Lengo lake kuu lilikuwa ni kuilazimisha Iran ikubali kutekeleza masharti 12 yaliyotakiwa na Marekani, ikiwa ni pamoja na kusimamisha mpango wake wa amani wa nyuklia, kusimamisha uimarishaji wa makombora na ushawishi wa siasa zake kieneo. Ili kufikia lengo hilo, utawala wa Trump ulitekeleza ugaidi wa kila aina ukiwemo wa kiuchumi na kimatibabu dhidi ya Iran kupitia vikwazo.
Licha ya madai ya mara kwa mara ya Wamagharibi hususan Marekani na utawala wa Kizayuni kuhusu juhudi za Iran za kutengeneza silaha za nyuklia, lakini mashirika ya ujasusi ya Marekani yenyewe yamatoa ripoti kadhaa yakisisitiza kuwa Iran haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia.
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, katika mazungumzo yake pembezoni mwa mkutano wa Davos mnamo Januari 21, 2025, akijibu swali kuhusu iwapo wakala huo unathibitisha madai ya utawala wa Kizayuni kwamba kuna malengo ya kijeshi katika mpango wa nyuklia wa Iran, alisema: "Hapana, hatuna ushahidi kwamba Iran inaunda silaha za nyuklia."
Kwa hakika tuhuma hizi zinatolewa katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza mara kwa mara kwamba sio tu kwamba haina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia, bali hata haifikirii kuelekea upande huo. Kinyume na tuhuma hizo zisizo na msingi za nchi za Magharibi kuhusiana na juhudi za Tehran kutengeneza silaha za nyuklia, Iran imeweza kutumia teknolojia ya nyuklia kwa kiwango kikubwa katika nyanja mbalimbali, zikiwemo za uzalishaji umeme, dawa, kuimarisha kilimo na mambo mengine. Kwa kutilia maanani kwamba Iran itahitajia umeme zaidi katika siku zijazo, inapasa iongeze kiwango cha umeme inaohitaji ukiwemo ule unaotokana na nishati ya nyuklia ili kukidhi mahitaji hayo.
342/
