22 Februari 2025 - 19:38
HAMAS: Mateka 6 Waisrael wataachiwa leo mkabala wa Wapalestina 602 walioko kwenye jela za Israel

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza majina sita ya mateka Waisrael, ambao wanatazamiwa kuachiliwa leo katika mwendelezo wa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kubadilishana mateka na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika taarifa iliyotoa Ijumaa, kupitia msemaji wake Abu Ubaidah, Hamas imesema, Eliya Cohen, Omer Shem-Tov, Omer Wenkert, Tal Shoham, Avera Mengistu na Hisham al-Sayed wataachiliwa leo.

Mkabala wake, utawala ghasibu wa Kizayuni utawaachilia huru Wapalestina 602 unaowashikilia kidhulma katika magereza yake.

Ikizungumzia utekelezwaji wa zoezi hilo linalotazamiwa kukamilishwa leo, Ofisi ya Habari ya Jumuiya inayoshughulikia masuala ya mateka wa Kipalestina imesema, mabadilishano ya leo yatakuwa ni ya saba katika awamu ya kwanza ya mchakato wa kubadilishana mateka.

Miongoni mwa mateka Wapalestina wanaotazamiwa kuachiliwa huru leo, 50 miongoni mwao wamekuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela na 60 wengine vifungo vya muda mrefu.

Mbali na hao, mateka wengine 47 Wapalestina ambao wataachiliwa huru ni waliokuwa wameachiliwa hapo awali chini ya makubaliano ya kubadilishana mateka yaliyojulikana kama "Wafa al-Ahrar" ya mwaka 2011, ambayo yalishuhudia mateka hao Wapalestina wanaachiliwa mkabala wa Hamas kumwachilia askari wa Israel Gilad Shalit, lakini baadaye jeshi la Kizayuni likawakamata tena Wapalestina na kuwarejesha magerezani.

Mateka wengine 445 wa Palestina kati ya 602 watakaoachiliwa leo ni wakazi wa Ukanda wa Ghaza, ambao walitiwa nguvuni na jeshi la utawala wa Kizayuni kufuatia vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala huo dhalimu dhidi ya Ghaza kuanzia Oktoba 7,2023.../

342/