22 Februari 2025 - 19:38
Israel yampiga marufuku msomi maarufu wa Kiislamu kuingia Msikiti wa Al-Aqsa

Vikosi vya utawala vamizi wa Israel vimemkamata na kumpiga marufuku Sheikh Najeh Bakirat, kiongozi mashuhuri wa Kiislamu Palestina kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa ulioko jijini Al Quds (Jerusalem).

Kulingana na Kituo cha Habari cha Palestina, vikosi vya Israel vilimkamata na kumhoji Sheikh Bakirat kabla ya kumpiga marufuku kuingia Msikiti wa Al-Aqsa kwa zaidi ya miezi sita.

Sheikh Najeh Bakirat ni naibu mkuu wa zamani wa Idara ya Wakfu wa Kiislamu katika mji wa Al-Quds unaokaliwa kwa mabavu. Alitekwa na polisi kutoka kwenye gari lake karibu na Lango la Al-Maghariba la msikiti huo.

Vyanzo vya ndani viliripoti kuwa maafisa wa polisi walitaifisha gari la Sheikh Bakirat na kumpeleka katika Kituo cha Kizuizi cha Moskobiya, ambako alisailiwa kwa takribani saa mbili kabla ya kupewa amri ya kutomruhusu kuingia Al-Aqsa kwa muda wa wiki moja.

Vikosi vya Israel pia vilimkamata mwana Sheikh Bakirat, Dawoud, katika moja ya milango ya kuingia Msikiti wa Al-Aqsa. Dawoud alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Qishla, ambako naye alikabidhiwa amri ya marufuku ya wiki moja kuingia msikitini.

Hivi karibuni pia, wakati mashambulizi ya jeshi katili la utawala haramu wa Israel katika sehemu mbalimbali za Ukingo wa Magharibi yakiendelea kwa zaidi ya mwezi mmoja mfululizo, vikosi vya utawala huo ghasibu vimevamia nyumba ya mhubiri wa Msikiti wa Al-Aqsa, Sheikh Ekrima Sabri.

Sheikh Sabri ni mkosoaji mkubwa wa uvamizi wa Israeli katika maeneo ya Palestina ambao umedumu kwa miongo kadhaa. Hapo awali, aliwahi kushikilia nafasi ya Mufti wa al-Quds na maeneo ya Palestina kuanzia mwaka 1994 hadi 2006.

342/