23 Februari 2025 - 19:24
Kiongozi wa Mapinduzi: Muqawama wa kukabiliana na ughasibu, dhulma na uistikbari si wa kumalizika

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma salamu na ujumbe maalumu kwa mnasaba wa kufanyika mazishi na maziko ya Mwanajihadi mkubwa Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na Shahidi Sayyid Hashim Safiyyuddin na kusisitiza kuwa: "adui ajue kwamba, Muqawama wa kukabiliana na ughasibu, dhulma na uistikbari si wa kumalizika; na kwa idhini ya Allah utaendelea hadi ufikie lengo ulilokusudia".

Kwa mujibu wa Pars Today ikinukuu IRNA, katika ujumbe wake huo aliotoa kwa mnasaba wa mazishi na maziko ya mwanajihadi mkubwa Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na Shahidi Sayyid Hashim Safiyyuddin, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaenzi Mashahidi hao wawili waadhamu wa Muqawama na akasema: "adui ajue kwamba, Muqawama wa kukabiliana na ughasibu, dhulma na uistikbari si wa kumalizika; na kwa idhini ya Allah utaendelea hadi ufikie lengo ulilokusudia."

Ujumbe kamili wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu uliosomwa leo kwa niaba yake katika mazishi hayo na Hujjatul-Islam Sayyid Mojtaba Hosseini, mwakilishi wake nchini Iraq na mjumbe wa wawakilishi wake Kiongozi Mkuu waliotumwa Lebanon, ni huu ufuatao:-

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

Amesema Mwenyezi Mungu Mwenye Izza na Aliyetukuka: "Na utukufu ni wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waumini, lakini wanafiki hawajui".

Mwanajihadi mkubwa na kiongozi wa mstari wa mbele wa Muqawama katika eneo, Maudhamu Sayyid Hassan Nasrullah (Allah Aipandishe Juu Zaidi Daraja Yake), sasa hivi yuko kwenye kilele cha izza na utukufu. Mwili wake safi unazikwa kwenye ardhi ya Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, lakini inshaaLlah, roho na njia yake itang'ara zaidi na zaidi kila siku na kuwamurikia njia wale wanaoifuata.

Adui ajue kwamba, Muqawama wa kukabiliana na ughasibu, dhulma na uistikbari si wa kumalizika; na kwa idhini ya Allah utaendelea hadi ufikie lengo ulilokusudia.

Jina jema na sura yenye nuru ya Janabi Sayyid Hashim Safiyyuddin (Radhi za Allah Ziwe Juu Yake) nayo pia ni nyota yenye kung'ara katika historia ya eneo. Yeye alikuwa msaidizi wa karibu na sehemu isiyotenganika ya uongozi wa Muqawama nchini Lebanon.

Amani ya Mwenyezi Mungu na waja wake wema iwe juu ya wanajihadi hawa wawili wenye kuheshimika na juu ya wapambanaji wengine mashujaa na waliojitolea, waliouawa shahidi hivi karibuni, na juu ya Mashahidi wote wa Uislamu. Na salamu zangu maalumu zikufikieni nyinyi wanangu wapendwa, vijana mashujaa wa Lebanon.

Sayyid Ali Khamenei 3/12/1403 Hijria Shamsia