Kwa mujibu wa IRNA, maelfu ya watu wameshiriki katika Sala ya kuwaombea Mashahidi Sayyid Hassan Nasralluh na Sayyid Hashim Safiyyuddin mjini Beirut.
Kwa mujibu wa Al-Mayadeen, Sheikh Muhammad Yazbek, Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei ndiye aliyeongoza Sala ya Maiti ya Mashahidi waadhamu wa Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon.
Shirika la habari la Reuters, limeakisi mazishi ya Mashahidi Sayyid Hassan Nasrullah na Sayyid Hashim Safiyyuddin na kuripoti kuwa: makumi kwa makumi ya maelfu ya watu wamekusanyika katika viunga vya Beirut leo (Jumapili) kutoa heshima zao kwa kiongozi wa Hizbullah Hassan Nasrullah.
Katika ripoti yake hiyo, Reuters limeweka picha za mazishi hayo makubwa na kueleza kwamba: wafuasi wa Hizbullah, wakiwa wameshikilia picha za Shahidi Nasrullah na bendera za harakati hiyo, walikusanyika Jumapili asubuhi kwenye uwanja wa michezo ulioko kwenye vitongoji vya kusini mwa Beirut, ambao unadhibitiwa na Hizbullah, kushiriki katika shughuli hiyo kubwa ya mazishi ya Nasrullah na viongozi wengine wa harakati hiyo waliouawa shahidi.
Shirika hilo la habari limeongeza kuwa uwanja huo wa Beirut unaobeba watu 55,000 ulikuwa takribani umeshajaa saa kadhaa kabla ya kuanza shughuli ya mazishi.
Tangu alfajiri ya asubuhi ya leo Jumapili, wananchi wa Lebanon walisafiri kutoka sehemu mbalimbali za nchi hiyo kwenda kushiriki kwenye mazishi ya Mashahidi Sayyid Hassan Nasrullah na Sayyid Hashim Safiyyuddin ili kuwaaga Mashahidi hao wawili watukufu na kutoa upya baia' na kiapo cha utiifu kwao.../
342/
