23 Februari 2025 - 19:27
Hamas yakadhibisha madai ya kuwauwa mateka wa Kizayuni

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amekadhibisha vikali madai ya uwongo ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba harakati hiyo imewauwa mateka wake kadhaa wa Israel.

Hazem Qasssim amesema kuwa Hamas inalaani madai ya uwongo ya adui Mzayuni kuhusu kuuliwa ndugu wa familia ya Shiri Bibas na jitihada za utawala wa Israel za kuiibebesha tuhuma Hamas.

Hazem Qassim ameongeza kuwa: Madai ya utawala wa Kizayuni kuhusu suala hilo ni ya uwongo na hayana msingi, na yametolewa ili kuharibu taswira ya harakati ya mapambano ya ukombozi wa Palestina na kuhalalisha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.

Msemaji wa Hamas amesisitiza kuwa: Muqawama ulilinda uhai wa mateka kwa kuwajibika, kudhihirisha uaminifu na kuzingatia kanuni na misingi ya maadili ya Kiislamu na kibinadamu.

Hazem Qassim amebainisha kuwa: Madai ya uwongo ya utawala wa Kizayuni ni jaribio lililofeli na kutaka kucheza na hisia za familia za wafungwa ili kubadili mkondo wa hasira na ghadhabu zinazoongezeka kila uchao za Wazayuni dhidi ya Benjamin Netanyahu na baraza lake la mawaziri la kigaidi na lenye misimamo mikali.

Brigedi za Izzudin Qassam jana ilikabidhi kwa wafanayakazi wa Jumuiya ya Msalaba Mwekundu miili minne ya mateka wa Israel. Hata hivyo utawala huo umedai kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa DNA kwenye miili hiyo, ilibainika kuwa moja ya maiti hizo haikuwa ya mateka wa Israel.

Katika kutoa maelezo ya kina kuhusu tukio hilo, Hamas imesema kuwa: Huwenda miili hiyo ilichanganyika pamoja kufuatia mashambulizi makali ya jeshi la utawala wa Kizayuni yaliyouwa mateka kadhaa wa Israel na raia wa Palestina, na kwamba itachunguza suala hili haraka iwezekanavyo.

342/