23 Februari 2025 - 19:29
WHO yasisitiza kuhusu makubaliano ya kuzuia majanga

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameonya kuwa historia haitazisamehe nchi ikiwa zitashindwa kuingia katika makubaliano ya kuzuia kwa pamoja majanga ya siku zijazo.

Kiongozi huyo wa WHO amesema hayo wakati wa kuhitimisha mazungumzo ya kutafuta makubaliano hayo kabla ya wiki ya mwisho ya mjadala katika makao makuu ya shirika hilo mjini Geneva, huku kukiwa na hatua kidogo za maendeleo zilizopigwa.

Ghebreyesus ameongeza kuwa, mataifa yalikuwa yamefikia kilele cha kukamilisha makubaliano hayo ya kihistoria ya kukabiliana na majanga ya siku zijazo kwa pamoja.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema kuwa, kumekuwa na hatua za maendeleo labda sio kwa kiwango kilichotarajiwa lakini akaongeza kuwa kuna matumaini.

Kadhalika amewaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba wako katika hatua muhimu wanapoelekea kukamilisha makubaliano ya majanga kabla ya kongamano la kila mwaka la maamuzi la WHO litakalofanyika mwezi Mei mwaka huu.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus alisisitiza kuwa shirika hilo haliegemei upande wowote wa nchi mwanachama na kwamba limeanzishwa kwa ajili ya kuhudumia nchi zote na watu wote.

“Kama shirika la UN, WHO haliegemei upande wowote na liko kwa ajili ya kuhudumia nchi na watu wote,” amesema Dkt. Tedros akiongeza kuwa, “nchi wanachama hutuuliza mambo mengi, na kila wakati tunajaribu kusaidia kwa kadri tunavyoweza.”

342/