Kamanda huyo wa Jeshi la Wanamaji amesema, “vikosi vya majini vya Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vipo katika Mlango-Bahari wa Malacca (Kusini-Mashariki ya Asia) na karibu na Ghuba ya Aden (kusini mwa Yemen), kiasi kwamba hivi sasa tumetuma kwa wakati mmoja msafara wa manowari nambari 5 za operesheni na utoaji mafunzo kwenye maeneo hayo ya baharini".
Admirali Shahram Irani ameongezea kwa kusema: "utekelezaji wa operesheni imara ya Jeshi la Kimkakati la Wanamaji kwenye eneo la pwani umeonyesha kuwa, tumefikia kiwango cha uwezo ambao umetufanya tuwe ngome imara ya pwani ya kuzuia uvamizi wowote unaoweza kufanywa baharini".
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi zilizoko kwenye eneo muhimu la baharini. Iran ina eneo la zaidi ya kilomita 5,800 za ukanda wa pwani, na karibu asilimia 40 ya mipaka yake ni ya baharini. Kwa kuzingatia pia kuwa, takribani asilimia 90 ya biashara za Iran zinafanywa kwa njia ya bahari, kwa hiyo uwezo wa Jeshi la Wanamaji una umuhimu mkubwa sana kwa mtazamo wa kijeshi na kiulinzi na kwa mtazamo wa kiuchumi pia.
Katika miaka ya karibuni na licha ya kuwepo vikwazo, Jeshi la Wanamaji la Iran limeongeza nguvu na uwezo wake kwa kutegemea uwezo wa ndani wa wataalamu wa Kiiran. Hivi sasa, Jeshi la Kimkakati la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lililojizatiti kwa manowari ya kubebea ndege zisizo na rubani na aina kadhaa za vyombo vipya vya majini vilivyoundwa ndani ya nchi, vikiwemo vya juu na vya chini ya bahari, limebadilika na kuwa nguvu kubwa katika eneo la Ghuba ya Uajemi na eneo huru la maji ya kimataifa, yenye taathira nyingi katika kulinda maslahi ya taifa, malengo ya kiulinzi na vilevile kukabiliana na ugaidi wa majini na kudhamini amani na usalama wa baharini.
Tokea tangu na tangu, Jeshi la Wanamaji la nchi yoyote ile limekuwa likizingatiwa kuwa moja ya nyenzo muhimu za kijeshi na kiuchumi; na hasa kwa kutilia maanani kuwa, katika karne za hivi karibuni, ili kuudhibiti ulimwengu, madola makubwa yamejaribu kuhakikisha kwamba, yanakuwa na majeshi ya wanamaji yenye nguvu kubwa ili kuendelea kuhodhi na kudhibiti masuala ya kijeshi na kiuchumi duniani.
Operesheni ya Msafara wa Manowari Nambari 86 wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyomalizika mwaka 2023, ilikuwa operesheni ya aina yake na ya nadra kushuhudiwa duniani na ilidhihirisha uwezo wa Iran katika medani ya baharini.
Msafara wa manowari hizo uliojumuisha manowari ya mashambulizi ya Dena na manowari-bandari ya Makran, ulizunguka dunia kwa mara ya kwanza kwa siku 213, na mnamo mwaka 2023, na baada ya kukata masafa ya kilomita 65,000 kuuzunguka ulimwengu na kuvuka Bahari za Hindi, Pasifiki, na Atlantiki uliwasili kwenye eneo la maji ya Iran.
Wakati wa operesheni yake hiyo ya kikazi, msafara huo wa manowari ulivuka mstari wa Ikweta mara nne na kutia nanga kwenye bandari za Mumbai, India, Jakarta, Indonesia, Rio de Janeiro, Brazil, Cape Town, Afrika Kusini na Salalah, Oman; na kupita pia kwenye Mlango-Bahari wa Malacca, Bahari ya Celebes, Bahari ya Pasifiki, Mlango-Bahari wa Magellan, Bahari ya Atlantiki, Bahari ya Hindi, na Bahari ya Oman.
Huo ulikuwa msafara wa kwanza wa kundi la manowari za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuizunguka sayari ya dunia kupitia Bahari ya Pasifiki na kuingia katika bara la Amerika, na kuonyesha uwezo wa wataalamu wa ndani na vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Msafara wa Manowari Nambari 86 wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulirejea kwa mafanikio katika eneo la majini la hapa nchini ili kuonyesha uwezo wa baharini wa Iran kwa madola makubwa duniani na kuandaa mazingira ya kuweza kunufaika na "uchumi wa baharini."
Mafanikio ya Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalipanuka baada ya operesheni za Msafara wa Manowari nambari 86, na hii leo Iran imekuwa na nafasi maalumu katika teknolojia ya sekta ya bahari duniani.
Ukweli ni kwamba, Jeshi la Wanamaji la Iran limeweza kukabiliana na ukiritimba wa Marekani na nchi za Magharibi kwa kupanua uwezo wake katika nyuga mbalimbali na kuonyesha nafasi na mchango wake athirifu katika kudhamini usalama wa njia za majini za kikanda na kimataifa…/
342/
