25 Februari 2025 - 17:32
HAMAS: Kuwa na silaha ni haki ya kisheria ya Muqawama na kuachana nazo ni jambo lisilowezekana

Hazem Qassem, msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ameashiria matamshi yaliyonasibishwa na kiongozi mwandamizi wa harakati hiyo Musa Abu Marzouk na kusisitiza kwamba: "Hamas inaendelea kutumia silaha za Muqawama kama haki halali na ya kisheria na haitalegeza msimamo juu ya suala hilo".

Hazem Qassem, amebainisha kuwa: "maadamu ukaliaji wa ardhi wa Palestina kwa mabavu ungali unaendelea, suala la silaha kwa ajili ya Muqawama halitakuwa la kujadiliwa kwa namna yoyote ile, na matamshi yanayonasibishwa na Musa Abu Marzouk sio msimamo rasmi wa Hamas.

Gazeti la New York Times linalochapishwa nchini Marekani limedai kuwa limemnukuu Abu Marzouk akisema: "Hamas iko tayari kufanya mazungumzo kuhusiana na silaha zake".

Msemaji wa Hamas ameeleza kwamba: mwenendo wa kichokozi na uharibifu wa Wazayuni maghasibu katika vita vyote dhidi ya mataifa ya eneo ndiyo sababu ya uharibifu mkubwa uliofanywa katika Ukanda wa Ghaza, na hivi sasa wavamizi hao wanaendelea kukamilisha sera hiyohiyo ya ubomoaji na uharibifu katika Ukingo wa Magharibi.

Qassem amesisitiza kuwa: Muqawama katika sura na aina zake zote utabaki kuwa haki halali na ya kisheria kwa wananchi wa Palestina hadi watakapojikomboa na kuweza kurejea katika ardhi zao, na hamasa ya Oktoba 7 ni nukta ya mabadiliko muhimu sana katika historia ya mataifa yote yaliyovamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi zao, na vilevile ni hatua muhimu sana kimkakati katika njia ya mapambano ya kitaifa ya Palestina.

Siku ya Jumanne, Ismail Ridhwan, afisa mwingine mwandamizi wa Hamas alitamka bayana kuwa: "silaha za Muqawama ni mstari mwekundu ambao hauwezi kujadiliwa".

Ridhwan amebainisha kuwa: "Wazayuni maghasibu wanafanya hila ili kukwepa kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano".

Kiongozi huyo wa Hamas ameongezea kwa kusema: "sisi tunatoa wito kwa pande za wapatanishi ziwashinikize wavamizi waheshimu na kutekeleza kikamilifu makubaliano ya kusitisha vita".../

342/