Ripoti hiyo ya The Economist imeeleza kwamba, kulingana na matini ya rasimu mpya ya mkataba uliopendekezwa na Marekani kwa Ukraine, Kyiv italazimika kulipa kwa mfuko mpya wa uwekezaji unaomilikiwa na serikali ya Marekani asilimia 50 ya mapato ya serikali yanayotokana na miundombinu yake na maliasili, kama vile bandari.
Kwa mujibu wa The Economist, afisa mmoja wa Ukraine amesema: “ikiwa tutatia saini rasimu hii katika hali yake ya sasa, kesho kundi la wahuni wenye hasira litatutupa nje ya ofisi zetu na kutunyonga.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mnamo Februari 20, Kiev ilipokea nakala ya makubaliano yake na Marekani ambayo imetajwa kuwa ni "janga kubwa zaidi," na ambayo imesimamiwa na waziri wa biashara wa Marekani Howard Lutnick. Gazeti la The Economist limeripoti kuwa, maafisa wa Ukraine wanaamini kwamba, Kiev itapokea rasimu ambayo ni “janga baya zaidi” kwa sababu ilikataa kutia saini rasimu zilizokuwa zimependekezwa hapo awali.
Mnamo Februari 3, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa, Washington inatarajia kwamba Kiev itatoa rasilimali zake adimu za madini, mkabala wa kupokea msaada wa kijeshi na kifedha kutoka nchi hiyo. Gazeti la Washington Post liliripoti Februari 14 kwamba wawakilishi wa Marekani katika mkutano na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Munich, walipendekeza kusainiwa waraka ambao ungeipa Marekani haki ya kutumia asilimia 50 ya rasilimali za madini ya nchi hiyo ambayo bado hayajachimbwa. Zelensky alitangaza baadaye kwamba alikataa kutia saini mkataba huo kwa sababu aliuhisi hauna manufaa na Ukraine.../
342/
