27 Februari 2025 - 20:06
Rais wa Iran ataka kuimarishwa uhusiano wa mataifa ya Waislamu

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema kuimarisha maelewano na uhusiano miongoni mwa nchi za Kiislamu zikiwemo Iran na Malaysia ni miongoni mwa mambo ya lazima katika hali ya sasa ya kimataifa.

Pezeshkian aliyasema hayo katika mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia, Dato' Seri Utama Haji Mohamad Bin Haji Hasan mjini Tehran Jumatano na kuongeza kuwa, "Kustawisha umoja baina ya viongozi na wanasiasa wa ulimwengu wa Kiislamu kutakuwa na nafasi muhimu sana katika kuondoa hitilafu, kutoelewana na umaskini katika mataifa ya Kiislamu.

Pezeshkian amesema, "Utawala wa Kizayuni (Israel) hivi sasa unathubutu kufanya jinai na uchokozi katika eneo (la Asia Magharibi) kwa sababu ya tofauti miongoni mwa Waislamu."

"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiandaa na inatilia mkazo upanuzi wa mawasiliano na ushirikiano na nchi za Kiislamu, ikiwemo Malaysia, katika nyanja zote," amesema.

Pezeshkian amezungumzia pia ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa eneo hili na kueleza kuwa jinai hizo zinatokea kwa sababu Waislamu wanahasimiana wao kwa wao.

Rais wa Iran amesisitiza umuhimu wa kustawisha umoja kati ya nchi za Kiislamu na kusisitiza kuwa utawala wa Kizayuni unafanya jinai kwa sababu ya mifarakano miongoni mwa Waislamu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia amesema uhusiano kati ya Tehran na Kuala Lumpur unatokana na maelewano na udugu baina yao.

Ameeleza nia ya Malaysia ya kuimarisha uhusiano na Iran na kutumia uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu katika nyanja za sayansi, teknolojia, kitaaluma, chakula na kilimo.

342/