27 Februari 2025 - 20:07
Baqaei: Kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kukomesha uvunjaji sheria wa Israel nchini Syria

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka kukomesha uvunjaji sheria wa utawala haramu wa Israel nchini Syria

Ismail Baqae sambamba na kulaani mashambulizi mapya ya anga na ardhini ya utawala ghasibu wa Kizayuni katika maeneo ya kusini mwa Syria na vitongoji vya Damascus, ametaka jumuiya ya kimataifa na nchi za Kiislamu kuchhukua misimamo ya dhati na imara katika kulaani hujuma hizo na kuchukua hatua za haraka za kukomesha uvunjaji sheria wa utawala huo ghasibu wa Kizayuni.

Akiashiria ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya mwaka 1974 unaofanywa na utawala wa Kizayuni, Baqaei ameutambua ukiukaji huo kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa misingi ya hati ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza kuwa, kukaliwa kwa mabavu sehemu za ardhi ya Syria na ukiukaji wa mara kwa mara mamlaka na umoja wa ardhi ya nchi hiyo ni sawa na kutenda jinai za kivamizi.

Baqaei amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua ya kusimamisha uchokozi na ukiukaji wa amani na usalama wa kimataifa unaofanywa na utawala wa Kizayuni.

Vyombo vya habari vya Syria Jumatano asubuhi vilitangaza kuwa sauti za milipuko mikubwa zimesikika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus. Tovut ya gazeti la al Watan pia imeandika kuwa, utawala wa Israel umeshambulia eneo la al Kiswah, kusini magharibi mwa Damascus. Aidha ndege zisizo na rubani za Israel ziliruka katika anga ya mikoa ya Quneitra na Dara'a, na kisha ndege za kivita za utawala huo zilishambulia eneo la "Tal al-Harah" katika mkoa wa Dara'a.

342/