27 Februari 2025 - 20:07
Iran yasambaratisha mtandao wa magaidi wakufurishaji na kunasa silaha nyingi

Katika operesheni kubwa ya kupambana na ugaidi, vikosi vya usalama vya Iran vimesambaratisha mtandao mkubwa wa magaidi wakufurishaji na kukamata silaha na mabomu kadhaa katika mkoa wa kusini-mashariki wa Sistan na Baluchestan.

Operesheni hiyo, iliyofanywa na idara ya usalama wa mkoa, ilipelekea kugunduliwa maghala manne yanayotumika kuhifadhi silaha na vifaa vya vilipuko vya kikundi hicho cha kigaidi.

Kulingana na vyombo mbalimbali vya habari nchini, maafisa wa usalama wa taifa wamekamata silaha nyepesi 226, zikiwemo bastola, bunduki za Kalashnikov na bunduki kubwa kama vile Goryunov.

Pia, wamepata vifaa vya kurusha makombora aina ya RPG, na zaidi ya kilo 20 za mabomu yakiwemo mabomu ya kutegwa barabarani (IEDs).

Wakuu wa usalama wamefichua kuwa silaha hizo zilikuwa zimeingia nchini kwa njia ya magendo, zikiwa zimefichwa ndani ya maboxi ya mafuta.

Magaidi hao wa kundi la wakufurishaji hivi karibuni wamejaribu kuvuruga usalama kusini-mashariki mwa Iran, kwa lengo la kuibua wahka, na kuzuia serikali kutoa huduma kwa wakazi wa mkoa huo.

Operesheni hii inafuatia mfululizo wa operesheni zingine za kupambana na ugaidi nchini Iran.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) hivi karibuni limevunja mtandao wa kigaidi unaohusishwa na Marekani na Israel katika Mkoa wa Mazandaran kaskazini mwa Iran, na kufichua njama zaidi za maadui za kuvuruga utulivu wa Iran.

Wakuu wa Iran wamekuwa wakiilaumu Marekani na washirika wake kwa kusaidia makundi ya kigaidi yanayolenga kuvuruga usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

342/