27 Februari 2025 - 20:07
Msikiti wa Mosalla Tehran kupanuliwa kuwa msikiti mkubwa zaidi duniani

Eneo kubwa la Swala la Tehran maarufu kama Mosalla Imam Khomeini litapanuliwa na kuwa msikiti mkubwa zaidi duniani.

Afisa mwandamizi wa kitengo cha ujenzi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), kinachojulikana kama Makao Makuu ya Khatam, alisema Jumatano kuwa Msikiti wa Mosalla litapanuliwa kwa hekta 200 kutokana na miradi inayoendelea hivi sasa

Mohammad Reza Rahmani, ambaye anaongoza kitengo cha usafiri na maendeleo ya miji cha Khatam amesema kwa vipimo hivi, Msikiti wa Mosalla utakuwa na eneo kubwa zaidi la Swala duniani. Amesema mradi huo pia utajumuisha majengo kadhaa ya shughuli za kidini na kiutamaduni.

Rahmani alisema kuwa Msikiti Mkuu wa Mosalla wa Tehran utaunganishwa na eneo kubwa la kijani katika kaskazini mwa Tehran, linalojulikana kama Chahar Bagh, kupitia daraja la lililojengwa juu ya Barabara ya Shahid Soleimani.

Amesema kuwa muunganisho huo utapanua eneo linaloweza kufikiwa la msikiti, na kuwapa waumini vivutio zaidi, ikiwa ni pamoja na maeneo zaidi ya maegesho ya magari.

Afisa huyo amesema kuwa ardhi zaidi katika eneo la Abbas Abad mjini Tehran zitanunuliwa na serikali ili kupanua eneo linalotumika la Mosalla.

Ujenzi wa Msikiti Mkuu wa Mosalla wa Tehran ulianza mapema katika miaka ya 1980 kwa pendekezo la viongozi wa kidini kwa lengo la kubadilisha mahali pa Swala ya Ijumaa kutoka Chuo Kikuu cha Tehran hadi eneo hilo pana.

Mradi huo baadaye ulipanuka na kuwa jumuiya kubwa ya kitamaduni, yenye kumbi ambazo huwa mwenyeji wa maonyesho makubwa ya kila mwaka na sherehe za kidini katika kituo hicho.

342/