27 Februari 2025 - 20:11
Mashtaka dhidi ya utawala wa Biden katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu

Taasisi ya "Demokrasia kwa ajili ya Ulimwengu wa Kiarabu Sasa" (DAWN), imefungua mashtaka dhidi ya Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden na mawaziri wake wawili yaani waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Anthony Blinken na waziri wa zamani wa ulinzi wa nchi hiyo Lloyd Austin katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ikiitaka ianzishe uchunguzi dhidi ya viongozi hao kutokana na kusaidia uhalifu wa kivita wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taasisi hiyo isiyo ya kiserikali lilianzishwa na Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari raia wa Saudia ambaye alikuwa pia mwandishi wa Middle East Eye na Washington Post. Khashoggi aliuliwa kikatili na maafisa wa Saudi Arabia ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo huko Istanbul, Uturuki, mwaka 2018. Taasisi ya DAWN inapigania demokrasia na haki za binadamu katika eneo la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini na inajitahidi kukomesha uungaji mkono wa Marekani kwa serikali kandamizi na zisizo za kidemokrasia za nchi za eneo hilo.

Ripoti ya kurasa 172 ya taasisi ya Dawn, inayoungwa mkono na mawakili waliosajiliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na wataalamu wengine wa masuala ya uhalifu wa kivita, inaonyesha kwamba viongozi wa zamani wa Marekani walikanyaga masharti ya Mkataba wa Roma na Mkataba wa Mahakama hiyo kwa kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni. Ripoti hiyo, iliyowasilishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, inabainisha kuwa Biden, Blinken na Austin waliunga mkono kisiasa na kijeshi jinai za Israel tena bila ya masharti yoyote wakati walikuwa wanafahamu kikamilifu kwamba Netanyahu, Gallant na wasaidizi wao wanatenda jinai za kutisha huko Ghaza.

Rais wa wakati huo wa Marekani, Joe Biden na maafisa waandamizi wa utawala wake, hususan waziri wa mambo ya nje, Anthony Blinken na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo, Lloyd Austin, ni washirika wa moja kwa moja katika jinai za Israel wakati wa vita vya Ghaza. Viongozi hao wa Marekani walisaidia kikamilifu jinai za Israel, kisiasa, kijeshi na silaha na waliusheheneza utawala wa Kizayuni kila aina ya silaha ili kuuchochea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wasio na hatia huko Ghaza.

Kwa upande wake, Taasisi ya Boston ya Marekani ilifichua katika ripoti yake kuwa, Marekani liunga mkono kikamilifu jinai za utawala wa Kizayuni wakati wa vita vya zaidi ya miezi 15 vya utawala huo dhalimu kwenye Ukanda wa Ghaza dhidi ya raia wasio na ulinzi. Rais mpya wa Marekani, Donald Trump pia amekubali kuipa Israel rundo jingine la silaha ambazo utawala wa Biden ulikuwa umesitisha kuupa utawala wa Kizayuni.

Taasisi ya DAWN imesema kuwa maafisa wa serikali ya Biden mara kwa mara walikwamisha kupasishwa vikwazo  dhidi ya Israel na badala yake waliupa utawala huo misaada ya kila namna licha ya kujua vyema kwamba misaada yao hiyo itachochea uhalifu wa kivita wa Israel huko Ghaza. 

Marekani ikiwa ni mshirika wa kimkakati wa utawala wa Kizayuni, ilichukua nafasi muhimu katika uvamizi wa utawala huo dhalimu kwenye Ukanda wa Ghaza wakati wa Joe Biden, kwa kutuma maelfu ya mabomu mazito ya kuvunja mahandaki na ya kuongozwa kwa mbali na kushiriki kikamilifu katika kuwaua shahidi maelfu ya wananchi wa Ghaza, hasa wanawake na watoto wadogo. Kwa kuzingatia yote hayo, tunaweza kusema kwa kinywa kipana kwamba Marekani ni mshirika wa moja kwa moja wa Israel katika jinai zake ambazo hazijawahi kushuhudiwa dhidi ya Wapalestina wa Ghaza na kwengineko ambako utawala wa Kizayuni unafanya jinai zake.

Kadhalika, licha ya kwamba jinai za utawala wa Kizayuni hususan mauaji ya kimbari ya watu wa Ghaza na kutumia kwake silaha ya kuwatesa kwa njaa na kiu Wapalestina zinalaaniwa kote ulimwenguni kiasi kwamba hata kumetolewa waranti wa kimataifa wa kutiwa mbaroni viongozi watenda jinai wa Israel, lakini Marekani si tu inapinga hatua hizoza kuiadhibu Israel, bali hata imekuwa ikichukua hatua dhidi ya kila taasisi inayotoa hukumu dhidi ya utawala wa Kizayuni. Pia Marekani imekuwa mara kadhaa inatumia kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuikingia kifua Israel na kuishajiisha iendelee kufanya jinai dhidi ya Wapalestina.


342/