3 Machi 2025 - 23:36
Source: Parstoday
Iran: Fedheha ya Zelensky nchini Marekani, kengele ya hatari ya kurejea ubabe wa karne ya 19

Iran imesema mwenendo wa kudhalilisha wa Rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, katika Ikulu ya White House unapaswa kuwa "kengele ya hatari" ya kurejea kwenye zama za karne ya 19 za uonevu na utumiaji mabavu katika uhusiano wa kimataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei ameyasema hayo leo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, siku tatu baada ya Trump kumfokea waziwazi Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wakati wa mkutano uliofanyika Ofisi ya Oval, White House akimlazimisha afanye makubaliano na Russia au apoteze uungaji mkono na himaya ya Washington.

"Kila mtu aliona suala hilo. Kila mtu anaweza kuwa na tafsiri yake ya mazungumzo na mijadala,” amesema Baqaei.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Ni kengele ya hatari na tunapaswa kujibu swali: Je, siasa za kimataifa zinarejea katika karne ya 19, wakati mabavu yalikuwa yakitawala mahusiano kati ya serikali? Vita viwili vikuu vya dunia na matokeo yake viliifanya jamii ya kimataifa ielewe kwamba matumizi ya nguvu yanapaswa kuzuiwa, na mahusiano yanapaswa kufanyika kwa mujibu wa sheria.”

Wakati wa majibizano makali ya Ijumaa iliyopita, Trump alimwambia Zelensky kwamba hana turufu wala hadhi ya kufanya maombi kwa Marekani, akimshutumu rais wa Ukraine kuwa hana shukrani kwa msaada wa kijeshi na kisiasa wa Marekani katika vita vya Ukraine na Russia.

Katika mazungumzo hayo ambayo yaligeuka na kuwa mabishano makali kati ya pande mbili mbele ya kamera za vyombo vya habari vya dunia, Trump na makamu wake walimdhalilisha waziwazi mgeni wao, huku Trump akimfokea Zelensky mara kwa mara.

Fukuto lilipozidi katika Ikulu ya White House, Volodymyr Zelenskyy alitoka kwa hasira bila kujibu maswali ya waandishi wa habari. Mkutano huo uliisha ghafla, huku Trump akifuta pia mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari uliokuwa umepangwa.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha