4 Machi 2025 - 23:25
Source: Parstoday
Madaktari wa Upasuaji wa Indonesia washangazwa na usahihi wa roboti za Iran

Roboti za upasuaji aina ya Sina, zinazotengenezwa nchini Iran na kusambazwa katika hospitali za Indonesia kwa madhumuni ya upasuaji, zimewashangaza wataalamu wa matibabu nchini humo.

Kulingana na ripoti iliyochapishwa na shirika la habari la Fars, madaktari wa upasuaji wanaofanya kazi na Mfumo wa Upasuaji wa Sina katika hospitali za Indonesia wameridhishwa na utendaji wa roboti hizo.

Ripoti hiyo ilisema kuwa takriban madaktari wapya 100 wa upasuaji nchini Indonesia wameomba kushiriki mafunzo ya kutumia mfumo wa Sina katika upasuaji wa mbali unaosaidiwa na roboti. Idadi hiyo ni juu ya madaktari  wengine 112 ambao tayari wamekuwa wakihudhuria mafunzo tangu mfumo huo ulipopelekwa Indonesia miaka miwili iliyopita.

Indonesia inatarajia kwamba mara baada ya kuidhinishwa, roboti za Sina zitaweza kusaidia kupanua Kituo cha Upasuaji wa Mbali kwa Roboti nchini humo, ili kuunganisha visiwa vya magharibi na mashariki vya nchi hiyo ambavyo masafa baina yao ni umbali wa kilomita 3,500.

Mfumo wa Sina, ambao umetengenezwa na kampuni ya roboti ya Iran, hutumia roboti kuiga harakati za mikono ya daktari wa upasuaji wakati wa operesheni.

Mfumo huu unatumia mbinu ya upasuaji isiyoingilia sana kwa kufanya upasuaji wa milimita tano kwenye sehemu ya mwili inayohitaji upasuaji. Hii inapunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kupona kwa mgonjwa baada ya operesheni na pia inaruhusu kushona jeraha kwa usahihi zaidi.

Roboti hizo huiga kila sentimita moja ya harakati za mikono ya daktari wa upasuaji kwa kusonga kwa milimita moja kwenye mwili wa mgonjwa. Mfumo wa roboti ya Sina ni matokeo ya takriban miaka 20 ya utafiti katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Tehran. Wataalamu waliohusika katika mradi huo wanasema kuwa kifaa hicho ni mfumo halisi wa Iran, kilichoundwa kwa kutumia utaalamu na teknolojia iliyotengenezwa na wahandisi na wanasayansi wa Iran.

Roboti hiyo imeshinda hataza 10 nchini Marekani na mataifa mengine, huku watafiti wakichapisha zaidi ya makala 70 katika majarida makubwa ya kisayansi ya kimataifa wakichambua mfumo huo.

Ripoti zinaonyesha kuwa mashirika yanayohusiana na serikali ya Russia pia yameonyesha hamu ya kununua roboti hiyo.

Your Comment

You are replying to: .
captcha