4 Machi 2025 - 23:31
Source: Parstoday
Baqaei: IAEA haipaswi kutoa maoni kwa mujibu wa matashi ya kisiasa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) haupaswi kotoa maoni kwa kuzingatia mitazamo ya kisiasa."

Esmail Baghaei ameyasema hayo akijibu ripoti ya hivi karibuni ya IAEA na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo akidai kwamba Iran inafanya jitihada za kupata bomu la nyuklia.

Baqaei ambaye alikuwa akizungumza jana Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran juu ya ripoti ya hivi karibuni ya IAEA na matamshi ya Mkurugenzi Mkuu wake ameongeza kuwa: "Matarajio yetu kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ni kwamba anafanya kazi ndani ya mipaka ya mamlaka na majukumu yake kwa mujibu wa sheria ya shirika hilo. Kutoa maoni kwa msingi wa uvumi na tetesi za kisiasa hakuko ndani ya mamlaka ya Mkurugenzi Mkuu wala hakusaidii kutatua lolote, na badala yake kunachochea anga na kuzuia mangiliano yenye kujenga."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Mpango wa nyuklia wa Iran umethibitishwa mara nyingi kuwa unatekelezwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.

Wakati huo huo Msemaji wa Kamisheni ya Usalama wa Kitaifa ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Wajibu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki si kujihusisha na masuala ya kisiasa, lakini sasa taasisi hii imekuwa chombo cha kisiasa cha nchi za Magharibi hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel."

Akijibu ripoti mpya ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu kasi ya Iran katika mchakato wa kuzalisha madini ya urani yaliyorutubishwa kwa kiwango juu, Ebrahim Rezaei amesema: "Ripoti hiyo bado haijachapishwa rasmi, lakini iwapo nakala ilivyowasilishwa katika baadhi ya vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi itakuwa ya kweli riipoti ya IAEA haitakuwa sahihi na itakuwa imetolewa kwa matashi ya kisiasa."

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha