Awamu ya kwanza ya usitishaji vita huko Gaza ilianza kutekelezwa Januari 19. Muda wa awamu ya kwanza ya makubaliano ulikuwa wa siku 42. Baada ya kukamilika kipindi hicho, utawala wa Kizayuni umekuwa ukivuruga na kukwamisha juhudi za kutekeleza awamu ya pili ya makubaliano hayo. Kanali ya 12 ya Televisheni ya utawala wa Kizayuni imedai kuwa, ujumbe wa mazungumzo wa utawala wa Kizayuni mjini Cairo utarejea Tel Aviv kutokana na upinzani wa Hamas wa kurefushwa awamu ya kwanza ya usitishaji vita. Hamas inataka kufanyika mazungumzo ya awamu ya pili ya usitishaji vita ambayo itahitimisha vita, huku utawala wa Kizayuni ukitaka kurefushwa awamu ya kwanza ya usitishaji vita.
Marekani sio tu kwamba inaunga mkono waziwazi utawala wa Kizayuni kwa kutaka kurefushwa awamu ya kwanza ya usitishaji vita, bali pia imewasilisha mpango kuhusu suala hili. Ofisi ya Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni ilitangaza mapema Jumapili kwamba baada ya mashauriano ya kiusalama yaliyoongozwa na Benjamin Netanyahu, iliamuliwa kuwa Israel itaidhinisha mpango wa mjumbe maalum wa Trump katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Wittkoff, wa kusitishaji vita kwa muda huko Gaza wakati wa Ramadhani na Siku Kuu ya Pasaka.
Pendekezo lililotolewa na mjumbe huyo wa Trump, halizungumzii kwa vyovyote vile masharti makuu yaliyotolewa na Muqawama kwa ajili ya kuachiliwa mateka wa Kizayuni waliosalia katika Ukanda wa Gaza, kama vile kusimamishwa kabisa vita, kuondoka kabisa askari wote wa utawala wa Kizayuni katika ukanda huo na kuanza mchakato wa kujenga upya ukanda huo. Kwa hivyo, mpango huo na kurefushwa kwa awamu ya kwanza ya usitishaji vita vimepingwa na Hamas. Kuhusiana na hilo Mahmoud Mardawi, mmoja wa viongozi wa harakati ya Hamas amesema: "Kamwe hatutakubali kurefushwa kwa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano, na kwa kuzingatia yale ambayo yametiwa saini, tunataka awamu zote za makubaliano hayo zitekelezwe."
Hitilafu hizo na uvurugaji wa pamoja wa Marekani na utawala wa Kizayuni umeupelekea utawala wa Kizayuni kuzuia kuingizwa Gaza bidhaa na misaada ya kibinadamu ili kuishinikiza Hamas. Shirika la Redio na Televisheni la Israel limeripoti kuwa, baraza la mawaziri la utawala huo limeamuru jeshi kufunga vivuko vyote vinavyoelekea Ukanda wa Gaza. Ripoti hii inaeleza kuwa uamuzi huo umechukuliwa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kwa ushirikiano na Wamarekani.
Katika kukabiliana na hatua ya Netanyahu ya kuzuia kuingizwa bidhaa na misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, ofisi ya vyombo vya habari ya serikali ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imesema: "Kuzuia misaada kuingia Ukanda wa Gaza kunamaanisha kulazimisha njaa dhidi ya wakazi wa ukanda huu, ambao wanategemea moja kwa moja misaada hii." Mahmoud Mardawi pia amesisitiza kuwa Netanyahu anadanganywa kuwa anaweza kufidia kushindwa kwake uwanjani kwa kuwatia njaa raia na kwamba anaweza kufikia malengo yake kwa njia hii, lakini kamwe hatutashinikizwa na hatutakubaliana na mpango huu. Kwa kuzingatia hali iliyojitokeza, wasiwasi wa kufeli usitishaji vita na kuanzishwa tena vita na baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni umeongezeka maradufu.
342/*
Your Comment