Baada ya kupanda miche hiyo, Imam Khamenei ameelezea upandaji miti kuwa ni hatua yenye faida, yenye mtazamo wa baadaye na inayozalisha utajiri. Pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia kwa uzito Harakati ya Kitaifa ya Upandaji Miti iliyozinduliwa mwaka jana katika serikali ya marehemu Shahidi Rais Ebrahim Raisi. Amesema kuwa watu wote wanapaswa kushiriki katika upandaji miti kama kitendo chema na kizuri, ili kwa kuongezeka miti, mazingira ya maisha yawe na uzuri na hewa safi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja upandaji wake wa miti kila mwaka kuwa ni ishara ya kukumbusha kuwa upandaji miti siyo tu kwa vijana, bali ni jukumu la watu wa rika zote. Amesisitiza kuwa kila mtu anapaswa kuwa na shauku na msukumo wa kushiriki katika kazi hii muhimu, kubwa na yenye uzuri.
Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa upandaji miti ni uwekezaji wenye faida kubwa kwa njia mbalimbali na ni njia ya kuzalisha utajiri. Ameongeza kuwa kupanda miti, iwe kwa ajili ya kupata matunda au kwa ajili ya matumizi ya mbao, ni jambo lenye faida kubwa na halina hasara yoyote.
Imam Khamenei ameendelea kubaini kuwa miti na mashamba ni vyanzo vya hewa safi na kusisitiza umuhimu wa mazingira, akibainisha kuwa miti na mimea husaidia siyo tu kuboresha hali ya hewa, bali pia huleta uzuri wa mazingira na faraja ya kiroho kwa binadamu, kwani miti na mimea ni ya kuvutia kwa macho na roho.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena umuhimu wa Harakati ya Kitaifa ya Upandaji Miti iliyoanzishwa wakati wa utawala wa marehemu Rais Shahidi Ebrahim Raisi, akisema kuwa mpango huo, ulioanza mwaka jana na unaoendelea, unaonyesha kuwa kupanda miti bilioni moja ndani ya miaka minne ni jambo linalowezekana. Amesitiza kuwa taasisi za serikali zinapaswa kuwasaidia wananchi katika juhudi hii.
Ayatullah Khamenei pia ametoa onyo dhidi ya ukataji miti kiholela na kubadilishwa matumizi ya ardhi za kilimo, akisema kuwa ukataji miti, isipokuwa kwa sababu maalum za kitaalamu na za lazima, ni kitendo chenye madhara na hatari. Amesisitiza haja ya kuzuia uharibifu wa misitu na uingizwaji wa ardhi za kilimo katika matumizi mengine.
Aidha, amerejelea kazi nzuri zilizofanywa katika jiji la Tehran na baadhi ya miji mingine katika ulinzi wa mazingira na upandaji miti, na kuhimiza kuendelezwa juhudi hizo.
342/
Your Comment