Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo katika khutba za Sala ya Ijumaa leo (Machi 7, 2025) iliyosaliwa kwenye Muswalla wa Imam Khomeini (MA) hapa Tehran na amezungumzia namna rais wa Marekani Donald Trump anavyomdhalilisha rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy na kusema: "Ulimwengu wote umeona fedheha na udhalilishaji ambao Trump amemfanyia rais wa Ukraine. Wale wote wanaojikomba kwa Marekani, wanapaswa kupata funzo kubwa hapo.
Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya hapa mjini Tehran pia amesema: Licha ya kwamba Kiongozi Muadhamu amekuwa akisisitiza sana kuwa, kufanya mazungumzo na Marekani si kuheshimika na wala si jambo la mantiki, lakini kuna baadhi ya watu ilikuwa inawawia vigumu kuamini. Hata hivyo hivi sasa na baada ya kuona udhalilishaji ambao Marekani imemfanyia rais wa Ukraine wanakiri kwamba mazungumzo na Marekani si katika hadhi ya taifa la Iran kwani kufanya mazungumzo na Marekani ni kujidhalilisha, ni kujidogesha na ni kupoteza heshima.
Ayatullah Khatami pia amesema: Marekani na troika ya Ulaya, yaani Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza, wameitishia Iran kwamba Baraza la Magavana la IAEA litalazimishwa kuchukua hatua dhidi ya Tehran lakini vitisho hivyo vimeshachakaa. Tunapaswa kusema kuwa, kwa zaidi ya miakaa 45 sasa wamekuwa wakitoa vitisho lakini wameshindwa. Baada ya hapa pia wataendelea kushindwa na tunatangaza hadharani kwamba kama hamtaachana na vitisho vyenu, basi taifa kubwa la Iran litaendelea kufelisha njama na vitisho vyenu vyote kupitia Muqawama wake wa kupigiwa mfano na litakufagieni kwenye medani na siasa zenu.
Amma kuhusu matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Imam wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesema: Hakan Fidan amedai kwamba Iran inapaswa kuacha siasa zake kuhusu eneo hili, bali hata ametuvunjia heshima. Kwanza anapaswa kuelewa kwamba siasa zetu ni za ujirani mwema na hatutarajii kabisa kugombana na majirani zetu, na hilo limeainishwa wazi kwenye Katiba ya Iran. Lakini pia matamshi yake ni ya kuvunja ujirani mwema na viongozi wa Uturuki waelewe kwamba matamshi kama hayo si kwa faida yao hata akidogo.
342/
Your Comment