8 Machi 2025 - 17:30
Source: Parstoday
Iran: Hakuna mazungumzo na Marekani wakati kuna vitisho na vikwazo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema Tehran haitashiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja kuhusu nyuklia na Marekani maadamu Washington inaendelea na vikwazo vya upande mmoja na vitisho.

Akizungumza Ijumaa na  shirika la habari la AFP pembeni mwa ziara yake mjini Jeddah, Aragchi amesema: “Hatuwezi kuingia katika mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani wakati wanaendelea na sera yao ya mashinikizo ya juu kabisa na vitisho vyao."

Araghchi, ambaye alikuwa  katika jiji hilo la Saudi Arabia ili kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), amesisitiza mtazamo wa amani wa Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia na kuwashauri watunga sera wa Marekani kufuata masharti ya “mazungumzo ya haki na ya usawa” badala ya kutumia lugha ya mashinikizo na vitisho.

Ameendelea kueleza kuhusu mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran na pande nyingine katika mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), zikiwemo Russia, China na nchi tatu za Ulaya.

Mahojiano hayo yalifanyika Ijumaa kufuatia madai ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kwamba alikuwa amemtumia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei. Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa na ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na Fox News, Trump alisema alitarajia kufanikisha makubaliano na Tehran kabla ya kutoa vitisho vya kijeshi dhidi ya nchi hii.  Mtawala huyo wa Marekani ametishia kuwa kama mazungumzo hayatafanyika atachukua hatua kwa kusema: "Njia nyingine ni kuchukua hatua, kwa sababu huwezi kuruhusu silaha nyingine ya nyuklia." Iran imesisitiza mara kwa mara kwamba haijawahi kutafuta mpango wa kuunda silaha za nyuklia.

Akijibu vitisho vya mara kwa mara vya kijeshi kutoka kwa Israel na Marekani dhidi ya mitambo ya nyuklia ya Iran, Araghchi amebainisha kuwa mpango huo hauwezi kuharibiwa kwa operesheni za kijeshi.
“Mpango wa nyuklia wa Iran hauwezi kuharibiwa kupitia operesheni za kijeshi… huu ni ujuzi tulioupata, na ujuzi huu uko kwenye akili za watu na hauwezi kushambuliwa kwa mabomu,” amesema.

Mbali na hayo, Aragchi amesema Iran ina uwezo wa kujibu uchokozi wa kijeshi  na kuongeza kuwa Waisraeli wenyewe wanajua, na wengine katika eneo hili wanajua, kwamba iwapo Israel itaishambulia Iran basi itapokea jibu kali na muafaka.

/

Your Comment

You are replying to: .
captcha