8 Machi 2025 - 17:39
Source: Parstoday
OIC yalaani njama za kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina Ghaza

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa taarifa rasmi mwishoni mwa kikao chake cha mjini Saudi Arabia na kulaani kwa nguvu zote njama za Marekani na Israel za kutaka kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.

Mkutano wa 20 wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC umefikia tamati usiku wa kuamkia leo Jumamosi mjini Jeddah, Saudi Arabia kwa kutolewa taarifa iliyoungwa mkono na washiriki wote wa mkutano huo. 

Katika taarifa hiyo, nchi wanachama wa OIC zimepinga vikali njama ya kulazimishwa kuhama Wapalestina na kusisitiza kuwa zinapinga kwa nguvu zote mpango huo.

Washiriki wa mkutano huo wamelaani vikali pia mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria na uvamizi wake dhidi ya ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu.

Taarifa hiyo pia imeidhinisha mpango wa Misri wa kujenga upya na kuboresha hali ya Ghaza wakati wa awamu ya kwanza ya kurejea wakimbizi kwenye maeneo yao.

Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu pia wametangaza kurejeshewa Syria uanachama wake katika jumuiya hiyo.

Kikao cha 20 cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ambacho ajenda yake ilikuwa ni "Uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina na njama za kulazimishwa Wapalestina kuondoka katika ardhi yao," kilifanyika jana Ijumaa, Machi 7, 2025 kwa pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kikao hicho kimefanyika katika makao makuu yake ya mjini Jeddah, Saudi Arabia.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha