9 Machi 2025 - 22:01
Source: Parstoday
Qalibaf: Iran haitasubiri barua yoyote kutoka Marekani

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema Jamhuri ya Kiislamu haisubiri barua yoyote kutoka kwa Marekani, kwani taifa hili linategemea uwezo wa ndani katika kukabiliana na changamoto zake.

Mohammad Baqer Qalibaf amesema hayo leo Jumapili katika kikao cha wazi cha Bunge, siku mbili baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kudai katika mahojiano na Fox News kwamba, amemtumia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei. Trump alidai kuwa ameionya Iran na kuitaka ihuishe mazungumzo ya nyuklia, au ikabiliwe kijeshi.

Spika wa Bunge la Iran amesema tayari imethibiti kwa taifa lenye hadhi la Iran kwamba, vikwazo vya maadui vinaweza tu kuondolewa kwa kuimarishwa zaidi uwezo wa Iran na kuongeza kuwa, hakuna mazungumzo yatakayopelekea kuondolewa vikwazo hivyo yanapoambatana na vitisho na ajenda ya Tehran kuwekewa mapatano mapya. 

Qalibaf amebainisha kuwa, tabia na mienendo ya Trump kwa nchi nyingine inaonyesha wazi kwamba wito wake wa mazungumzo ni hadaa na "udanganyifu" unaokusudiwa "kuipokonya silaha" Iran.

Spika wa Bunge la Iran ameeleza bayana kuwa: Hatusubiri barua yoyote kutoka kwa Marekani, na tunaamini kwamba, kwa kutumia uwezo na fursa za ndani kwa ajili ya kuendeleza uhusiano wa kigeni, tunaweza kufikia msimamo ambao adui hatakuwa na budi ila kuondoa vikwazo ndani ya fremu ya mazungumzo na pande zilizosalia za JCPOA.

Ikitoa radiamali yake kwa madai ya karibuni ya Trump, Tehran imesisitiza kuwa haijapokea barua yoyote kutoka kwa Marekani. Akizungumza jana Jumamosi, Kiongozi Muadhamu alisema sisitizo la baadhi ya madola ya kiistikbari la kufanya mazungumzo na Iran halilengi kutatua masuala yaliyopo, bali ni kutaka kutwishana matarajio yao. 

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha