12 Machi 2025 - 18:23
Source: Parstoday
Jamaatul-Islami yaitahadharisha serikali ya Pakistan isihadaiwe na hila za Trump

Mkuu wa Chama cha Kiislamu cha Jamaat-e-Islami Pakistan (JIP) ameihutubu serikali ya Islamabad akisema: Marekani si yenye kuitakia kheri katu Pakistan na haipasi kuridhia matakwa ya nchi hiyo.

Hafiz Naeem-ur-Rehman, Amir wa Jamaat-e-Islami Pakistan, amelaani jinai zilizofanywa Marekani katika eneo hususan moto wa vita uliowashwa na nchi hiyo nchini Afghanistan, na akaipa indhari serikali ya Waziri Mkuu Shehbaz Sharif ya kupata funzo na ibra kutokana na hatima ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na kutohadaiwa na kauli za kupongezwa na kusifiwa na Rais wa Marekani Donald Trump.

Hafiz Naeem-ur-Rahman ameeleza hayo alipotoa mjibizo kwa madai ya serikali ya Trump kwamba imemwinda na kumnasa mhusika mkuu wa shambulio la uwanja wa ndege wa Kabul kwa ushirikiano wa Pakistan, na akasema: "lengo kuu la Wamarekani nchini Afghanistan ni kuchochea na kuwasha moto wa vita, mauaji, umwagaji damu na kuzisambaratisha nchi za eneo hili".

Amir wa Jamaat-e-Islami Pakistan ameongeza kuwa: "Wamarekani ndio chimbuko kuu la ugaidi, misimamo mikali na ya kufurutu mpaka na kuuliwa kwa halaiki watu wasio na hatia; na sasa hivi wanatoa kauli za kuwasifu na kuwaenzi watu wengine kwa ajili tu ya kufikia malengo yao".

Wiki iliyopita, Rais wa Marekani Donald Trump alidai katika hotuba yake mbele ya Bunge la nchi hiyo Kongresi kwamba, kwa ushirikiano wa Pakistan, wamemkamata mwanachama wa DAESH (ISIS) aliyehusika na shambulio la uwanja wa ndege wa Kabul mnamo mwaka 2021.

Mtu huyo anayeitwa Mohammad Sharifullah, alikamatwa na vyombo vya intelijensia vya Pakistan karibu na mpaka na Afghanistan na hivi karibuni alikabidhiwa kwa serikali ya Marekani.

Baadhi ya wataalamu wa mambo nchini Pakistan wametilia shaka madai kwamba Sharifullah alikuwa na nafasi na machango mkubwa katika kupanga mashambulizi ya DAESH.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha