Baada ya Donald Trump kuingia tena Ikulu ya White House, kwa mara nyingine tena suala la uhusiano wa Marekani na Iran limekuwa kadhia nzito katika kauli za Rais mpya wa Marekani. Kama ilivyokuwa katika muhula wake wa kwanza wa urais kati ya 2016 na 2020, Trump amepitisha sera ya mashinikizo ya juu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa upande mmoja, Rais huyo wa Marekani anashinikiza kufanyika mazungumzo ya kutatua changamoto na Iran, na kwa upande mwingine, anatishia kutumia chaguo la kijeshi ikiwa mazungumzo hayatafanyika.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikionyesha na kuthibitisha kwamba iko tayari kuzungumza na kujadiliana, hata hivyo, kanuni kuu katika mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni "izza na kuheshimiana". Heshima, hekima na maslahi ni misingi mikuu mitatu ya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambazo ziliamuliwa na Kiongozi wa Mapinduzi. Msingi wa izza na kuheshimiwa unapaswa kuzingatiwa katika mazungumzo yoyote. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakubali kufanya mazungumzo ya aina yoyote yatakayovunja heshima na izza yake hata kama itakuwa chini ya mashinikizo ya kiuchumi kutokana na siasa za kihasama za maadui zake hususan vikwazo vya kikatili vya nchi za Magharibi hususan Marekani. Inatupasa kusema kuwa, matamshi ya vitisho ya Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanatokana hasa na mambo mawili: Mtazamo wake potofu kuhusu Serikali ya Iran na pia sera yake ya vita vya kiutambuzi na ufahamu (Cognitive Warfare) dhidi ya maoni ya umma nchini Iran.
Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika ujumbe wake akijibu matamshi ya vitisho ya Trump kuhusu kuilazimisha Iran kufanya mazungumzo kwamba: "Mazungumzo ni tofauti na utumiaji wa mabavu na kushurutisha. Hatutafanya mazungumzo chini ya mashinikizo na vitisho. Mazungumzo kama hayo hayafai hata kujadiliwa, haijalishi ni mada gani (ya kujadiliwa)."
Suala jingine ni kwamba, mazungumzo yanayokubalika na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mazungumzo ambayo yanaambatana na kuheshimiana. Kimsingi, Jamhuri ya Kiislamu inatilia mkazo ulazima wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala ya nchi zote na kuheshimiana katika mazungumzo na majadiliano. Ni vyema kusema hapa kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijafunga mlango wa mazungumzo na Marekani, lakini ifahamike kwamba sharti la mazungumzo ni kuheshimiana. Kuhusiana na suala hilo, Sayyid Abbas Araqchi ameashiria mazungumzo ya Iran na nchi tatu za Ulaya na vilevile na China na Russia na kuandika: "Hivi sasa tunafanya mazungumzo na nchi tatu za Ulaya - na Russia na China - kila moja kivyake katika mazingira sawa na kwa kuheshimiana. Huko nyuma, kila mara Marekani ilipowajihiana na Iran kwa heshima katika mazungumzo, ilipokea heshima; na kila ilipochukua misimamo ya vitisho, ilikabiliana na jibu la Iran. Kila tendo lazima kiwe na radiamali yake."
Suala jingine ni kwamba, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mazungumzo yanayokubalika ni yale yatakayoishia kwenye mapatano yenye kujenga kwa pande husika, na wakati huo huo kuwa na dhamana ya kiutendaji. Vinginevyo, mazungumzo kama hayo huwa ni kupoteza muda tu na hata kuigharimu nchi.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kupunguza mvutano na kutatua hitilafu na ukosefu wa maelewano kwa njia ya mazungumzo, lakini haijali wala haitetereshwi na vitisho vya matokeo ya kutofanya mazungumzo na upande wowote. Katika muktadha huu, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amekosoa vikali mwenendo wa kimaksi wa utawala wa Donald Trump dhidi ya Iran na kueleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu sio Ukraine, na katu haitafanya mazungumzo na Marekani katika mazingira ya vitisho au kulazimishwa.
"Lazima tudumishe uhusiano na ulimwengu. Hatutaki kutengwa au kugombana na mtu yeyote, lakini hiyo hii haina maana kwamba tutainama kwa udhalili mbele ya mtu yeyote," amesisitiza Rais Pezeshkian na kuusema: "Tuko tayari kufa kwa heshima, lakini hatutaishi kwa udhalili."
342/
Your Comment