15 Machi 2025 - 21:48
Source: Parstoday
Utawala wa Trump kuwapiga marufuku au kuwawekea mpaka wa kuingia Marekani raia wa nchi 43

Gazeti la New York Times limeandika katika toleo lake la leo kuwa serikali ya Donald Trump inapitia mpango wa kuwapiga marufuku au kuwawekea mpaka wa kuingia Marekani raia wa nchi 43.

Duru za kuaminika zimelieleza gazeti hilo kwamba, kwa mujibu wa rasimu iliyotayarishwa na maafisa wa usalama na wanadiplomasia, orodha hiyo ina sehemu tatu, ambazo ni nyekundu, chungwa na njano.

Katika orodha ya rangi "Nyekundu", kuna raia wa nchi 11 ambao watapigwa marufuku kikamilifu kuingia Marekani. Raia hao ni wa Afghanistan, Bhutan, Cuba, Iran, Libya, Korea Kaskazini, Somalia, Sudan, Syria, Venezuela na Yemen.

Katika orodha ya rangi ya "Chungwa", raia wa nchi 10 watawekewa mipaka maalumu ya kuingia Marekani. Raia hao ni kutoka Belarus, Eritrea, Haiti, Laos, Myanmar, Pakistan, Russia, Sierra Leone, Sudan Kusini, na Turkmenistan.

Kwenye orodha hiyo ya rangi ya Chungwa, watu wanaotaka kusafiri kuelekea Marekani kwa ajili ya shughuli za kibiashara yamkini wataruhusiwa kuingia nchini humo, lakini wahamiaji kutoka nchi hizo watazuiwa kuingia na utoaji viza za utalii kwa raia wa nchi hizo utafutwa.

Mbali na hayo, katika orodha ya rangi ya "Njano", ambayo inajumuisha nchi 22 ikiwemo Cameroon, Cambodia, Malawi na Mali, waombaji wanaotaka kuingia Marekani watatakiwa ndani ya muda wa siku 60 wawe wamesharekebisha masuala ambayo kwa mtazamo wa Marekani yana mapungufu. Vinginevyo, watahamishwa kwenye orodha ya rangi ya Chungwa au Nyekundu.

Duru za habari zimeeleza kuwa orodha hizo tatu zilitayarishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani wiki chache zilizopita na zina uwezekano wa kufanyiwa mabadiliko.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha